MAPENZI: Ikiwa hatengi muda kuwa nawe, hakupendi
KATIKA mahusiano ya ulimwengu wa sasa, kila mtu anatafuta kitu tofauti: mapenzi ya kweli, uaminifu, usalama wa kihisia au hata starehe za muda mfupi.
Lakini mojawapo ya dalili kuu za upendo wa kweli ni muda. Ndio, muda ni kipimo muhimu cha mapenzi ya kweli.
“Kama unapenda mtu, unataka kuwa naye. Kama anakupenda, atataka kuwa nawe. Hata akiwa na ratiba ngumu kiasi gani, atatafuta muda – hata kama ni dakika chache tu – kuzungumza nawe, kukuona, au hata kukutumia ujumbe wa kukupa matumaini,” asema mtaalamu wa mahusiano Joyce Kimanzi.
Lakini kama mtu anakupuuza kila wakati, kila mara ana visingizio vya “nimekuwa busy”, “leo siwezi”, “nimechoka”, “niko na shughuli nyingi” na haweki juhudi kuwa karibu nawe, huo sio upendo.
“Kama uko kwenye uhusiano lakini mtu wako hajawahi kukualika mtoke pamoja, kutembeleana, au hata kukukupigia simu kwa hiari hapo hakuna penzi la dhati,”asema. Pengine unamsaidia kifedha, kihisia, au unampa starehe fulani.
Lakini kila ukihitaji msaada, hauko kwa orodha ya vipaumbele vyake. Hajali hali zako, ila anajitokeza akihitaji kitu kutoka kwako, iwe ni msaada, pesa, au mahitaji ya kimwili. Ukimaliza kumpa, anaingia mitini hadi atakapohitaji. Huyo anakutumia, aeleza Kimanzi.
Mwanasaikolojia Swaleh Kamoni asema kuna watu wanaopiga simu au kutuma ujumbe tu kwa sababu wanahitaji kitu ilhali wanadai wako katika uhusiano wa kimapenzi nawe.
“Hawatoi salamu bila sababu. Ukimhitaji, haonekani. Ukimhitaji kwa jambo la dharura, hana muda. Mapenzi ya kweli huonekana kwa vitendo. Hakuna mtu aliye busy 24/7 kwa mtu anayemjali. Kama mtu anaweza kukaa siku nzima bila hata kukutumia ujumbe mfupi wa kukuuliza ukoje, ni wazi kuwa hauko katika moyo wake uko kwenye orodha ya akiba, si kipaumbele,” asema
Watalaamu wanasema watu wengi hukwama katika mahusiano ya muda mrefu wakitegemea kwamba mtu atabadilika. “Ukweli mchungu ni huu: mtu akikupenda kweli, hautalazimika kumuomba muda au kuomba thamani. Atakupa kwa hiari,” asema Kimanzi
Kamoni anashauri: “Usikubali kuwa ‘chaguo la pili’ kwa mtu ambaye ni “wa kwanza” kwako. Ukijikuta ukituma ujumbe mara kumi bila jibu, au kila mara unalazimika kuuliza “una muda lini tuonane?”, ni wakati wa kurudi nyuma na kujiuliza: Je, huu uhusiano ni wa kweli au ni mtego wa kihisia?”
Kulingana naye, mahusiano yanapaswa kujengwa juu ya msingi wa kuheshimiana, kutengeana muda, na mapenzi ya kweli. Kama huoni hayo – na kila unachopata ni visingizio na kupuuzwa – basi ni wakati wa kujiokoa. Usikubali kutumiwa kwa jina la mapenzi.
“Mtu asiyetenga muda wa kuwa nawe, anakwambia moja kwa moja bila kusema: ‘Sikupendi.’ Chukua hatua. Jithamini.