Pambo

Sheria kuhusu idhini ya mke au mume katika uuzaji wa mali ya ndoa

Na  BENSON MATHEKA August 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Sheria inawapa wakopeshaji au mtu yeyote anayepanga kununua ardhi inayotambuliwa kuwa mali ya ndoa, jukumu la kuuliza kutoka kwa mmiliki aliyesajiliwa iwapo mke au mumewe amekubali mpango wa kuiuza au kuikodisha ardhi hiyo.

Mmiliki aliyesajiliwa ana jukumu la kutoa taarifa sahihi kuhusu hali yake ya ndoa – kama ameoa/ameolewa au la. Ikiwa hajaoa au hajaolewa, anaweza kutakiwa kuapa kuwa yeye ni mke/mume asiye katika ndoa, ni mtalaka au ni mjane.

Iwapo kutatokea udanganyifu au utoaji wa taarifa za uongo kuhusu hali ya ndoa ya mmiliki aliyesajiliwa, mpango wa kuuza au kuhamisha ardhi hiyo unaweza kufutwa na mwenzi wake ambaye hakushirikishwa wala kutoa idhini yake.

Mwenzi ambaye hakutoa idhini anaweza kwenda mahakamani kuomba uuzaji ufutwe. Katika hali hiyo, mwenzi huyo huomba mkataba wowote wa uuzaji bila idhini yake utangazwe kuwa batili, na ikiwa kuna uhamishaji wa umiliki uliofanyika, ubatilishwe.

Sheria inataka idhini ya mwenzi iwe kwa maandishi na iwe ya hiari na ya kufahamu. Mwenzi anayetoa idhini ana haki ya kupata ushauri wa kisheria huru ili kuelewa asili ya muamala huo na athari zake kisheria.

Idhini hiyo haipaswi kutolewa chini ya shinikizo, udanganyifu, au ushawishi usiofaa. Ikiwa idhini ilipatikana kwa njia hizo, uuzaji unaweza kufutwa kwa ombi la mwenzi asiye na hatia.

Ruhusa ya mwenzi wa ndoa ni muhimu katika uuzaji au uhamishaji wa mali ya ndoa kwani hufanya muamala huo kuwa halali. Sheria ya Ardhi, kupitia Kifungu cha 79(3), inasema kuwa hati ya dhamana kuhusu mali ya ndoa ni halali tu ikiwa imesainiwa na wandoa wote au kuna hati inayoonyesha idhini ya mke au mume.

Katika kesi ya Mugo Muiru Investments Limited dhidi ya E W B & Wengine 2 (2017), Mahakama ya Rufaa iliamua kuwa:

“Ingawa mali ya ndoa ilikuwa imesajiliwa kwa jina la S.B. pekee, alishikilia hatimiliki na umiliki wa kisheria kwa niaba ya wote wawili – yeye na  mkewe – kwa pamoja. Kauli hii iliungwa mkono na uamuzi wa kesi ya Gissing dhidi ya Gissing (1970)

Jaji Lord Diplock katika kesi ya Gissing v. Gissing alisisitiza kwamba hata ikiwa mali imesajiliwa kwa jina la mmoja wa wenza, inaweza kuwa ni mali ya ndoa inayoshikiliwa kwa niaba ya wote wawili ikiwa kuna ushahidi wa uaminifu wa pamoja