Ndoa za kisiasa za Bonde, Mlima na Ziwa zinavyoathiri Kenya
KATIKA historia ya siasa za Kenya, miungano wa maeneo matatu muhimu ya kisiasa, Mlima, Ziwa, na Bonde, umekuwa ukiamua hatima ya uchaguzi mkuu, hasa wa urais.
Muungano wa viongozi kutoka maeneo haya huamua mwelekeo wa mamlaka, ushawishi wa kisiasa, na mikakati ya uchaguzi inayobadilika kila baada ya miaka mitano.
Tangu enzi za vyama vya siasa vya jadi kama KANU na FORD, hadi miungano ya hivi punde kama Jubilee, NASA na Kenya Kwanza, ni wazi kuwa yeyote anayetaka kushinda urais lazima ajue jinsi ya kuvutia Mlima, Ziwa na Bonde kwa wakati unaofaa.
Mwaka wa 2022, maeneo ya Mlima (Mlima Kenya) na Bonde (Bonde la Ufa) yaliungana chini ya muungano wa Kenya Kwanza, na yakampa ushindi Rais William Ruto.
Aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, alipewa unaibu rais serikalini kama ishara ya uthibitisho wa ushirikiano huo.
Lakini hali imebadilika kwa kasi. Tangu mzozo wa wazi kati ya Rais Ruto na Naibu wake Gachagua, Mlima umeanza kulegeza ushawishi wake ndani ya serikali.
Gachagua amekuwa akishinikiza ajenda ya ‘maslahi ya eneo la Mlima’, huku akitumia majukwaa ya kisiasa ndani na nje ya nchi kueneza ujumbe wa upinzani dhidi ya aliyekuwa mshirika na bosi wake.
Kauli kama “Wantam”—yaani muhula mmoja kwa Rais—zinazidi kusikika, zikiashiria kuwa Mlima Kenya huenda ukamtema Ruto kabla ya 2027.
Hii ni ishara kwamba salamu za Mlima si tena za kheri kwa Ruto, bali za mashaka.
Uhusiano wa Mlima na Ziwa (eneo la Ziwa Victoria, hasa Nyanza) huja kwa kutotarajiwa. Mwaka 2018, Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga waliweka historia kwa Handisheki, ushirikiano uliounganisha Mlima na Ziwa, huku ukimwacha Ruto pembeni.
Muungano huo ulizaa mpango wa BBI, uliolenga kubadilisha muundo wa serikali lakini ukapingwa na Mahakama. Hata hivyo, ulikuwa na athari kubwa kisiasa uliweka wazi kuwa Mlima na Ziwa zikishikana, wanaweza kutikisa siasa za kitaifa.
Baada ya kutofautiana na Gachagua, Ruto alirudi eneo la Ziwa alivyofanya mtangulizi wake Kenyatta na kujenga ukuruba wake wa sasa na Raila Odinga.
Mwaka 2022, hata baada ya Uhuru kumuunga Raila, Mlima uligeuka na kumchagua Ruto. Lakini hali ya sasa inaonyesha kuwa Mlima haujaridhika, na Raila, ambaye sasa yuko katika ushirikiano na Ruto, anaonekana kurejesha ushawishi Ziwani kupitia mlango wa nyuma wa mamlaka.
Bonde la Ufa limekuwa ngome thabiti ya Ruto tangu enzi za muungano Jubilee wake na Kenyatta. Ruto bado anaungwa mkono sana Bondeni. Hali hii inampa nafasi ya kuendelea kuwa na msingi imara wa kisiasa, hata kama Mlima unamtema.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa siasa, Kefa Oriae Bonde lina umuhimu mkubwa katika hesabu ya kura.
Kwa kuendelea kuthibiti Bonde, na kupata kiasi fulani cha uungwaji mkono kutoka Ziwa au Pwani, Ruto anaweza kuendelea kuwa na nafasi nzuri kisiasa hata kama Mlima utamtelekeza.
“Siasa za Kenya hazitegemei tena kikamilifu ukabila. Ruto anaonekana kubadilisha mbinu kwa kuwekeza kwa maeneo, wanawake na vijana. Fedha za wanawake na mikopo ya vijana zimesambazwa kwa wingi, huku serikali ikitumia mashinani kuimarisha uhusiano wake na wananchi wa maeneo muhimu,” asema Oriae.
Anasema huu ni mkakati unaolenga kuvunja ukabila na kuunda wigo mpya kuvutia kura kwa kutegemea ngome za jadi.
“Rais anaonekana kujishindia umaarufu katika zilizokuwa ngome za Raila za Nyanza na Magharibi na kwa kiwango kikubwa pwani. Kama Rais ataweza kuwavuta Gen Z waliompinga, pamoja na wanawake wanaowakilisha zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura, atakuwa amebadili mchezo kabisa.
Ushirikiano kati ya Ziwa na Bonde hauwezi kupuuzwa. Ni muungano wenye nguvu ambao unaweza kubadilisha siasa za Kenya.
Oriae anasema ushirikiano huo ulijaribiwa katika uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo nusura umwangushe Rais Mwai Kibaki katika uchaguzi wa mwaka huo uliozua umwagikaji mkubwa wa damu kuwahi kushuhudiwa nchini.
Wakati mwingine viongozi kutoka maeneo haya huleta salamu za maridhiano; wakati mwingine ni onyo. Lakini daima, ni ishara ya mabadiliko makubwa ya kisiasa.