Habari

Koome aponyoka jaribio la kung’olewa mamlakani

Na JOSEPH WANGUI August 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUME ya Huduma za Mahakama (JSC) imetupilia mbali matakwa kadhaa kuhusu kutimuliwa kwa majaji sita, akiwemo Jaji Mkuu Martha Koome, kwa kutotimiza vigezo vya kikatiba kufanikisha kuondolewa kwao.

Majaji wengine walioponea ni; Jaji wa Mahakama ya Juu Isaac Lenaola, Majaji wa Mahakama ya Rufaa Asike Makhandia na Kathurima M’Inoti na Jaji wa Mahakama Kuu Alfred Mibeya.

Malalamishi dhidi ya majaji hao yaliwasilishwa na aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Nelson Havi, mfanyabiashara Edwin Dande, Victoria Naishorua na kampuni ya Benjoh Amalgamated and Muiri Coffee Estate inayohusishwa na Kapteni (mstaafu) Kung’u Muigai.

Bw Havi alitaka kutimuliwa kwa Jaji Mkuu Koome, akimtuhumu kwa mienendo mibaya ya kuteua jopo la majaji watatu kusikiza kesi ambayo yeye na wenzake waliwasilisha dhidi ya JSC.

Bw Havi alisema Koome alipasa kuacha kibarua hicho kitekelezwa na mwengine, asije akashiriki mgongano wa kimaslahi.

Hata hivyo, JSC ilisema kuwa ni Jaji Mkuu pekee aliye na mamlaka ya kuteua jopo la majaji wa kusikiza kesi, kulingana na Kipengele cha 165 (4) cha Katiba.

Tume hiyo ilirejelea uamuzi wa juzi wa Mahakama ya Juu, uliokariri msimamo huo, ikisema hatua ya Koome iliafiki hitaji la katiba.

“Ombi hilo liliwasilisha mbele ya tume katika mkutano wake wa Julai 30, 2025. Na baada ya kujadiliana, tume ilifikia uamuzi kwamba halikutimiza viwango vya kufanikisha kuondolewa afisini kwa Jaji chini ya Kipengele cha 168 cha Katiba,” akasema Katibu wa JSC Winfrida Mokaya.

JSC pia ilitupilia mbali madai kuwa Koome aliteua majaji wasio na uzoefu mkubwa na waaminifu kwake.

Tume ilisema kuwa teuzi za majaji hufanywa na wanachama kwa pamoja wala sio kwa misingi ya uaminifu kwa mwanachama mmoja, akiwemo Rais wa JSC.

“Kwamba baadhi ya majaji waliteuliwa wakati ambapo Koome alikuwa Rais wa JSC hakumaanishi kuwa hawawezi kuamua kesi kwa njia huru, haki na bila mapendeleo,” tume ikasema.

Victoria Naishorua alipinga wajibu wa Jaji Lenaola kama msimamizi wa mali ya mwanasiasa wa zamani marehemu John Keen.

Lakini JSC ilikataa kushughulikia ombi hilo ikidai suala hilo tayari liko mbele ya Mahakama Kuu, kama kesi ya Urithi nambari 123 ya 2017.

“Kwa hivyo, tume hiyo ilisema haima mamlaka ya kushughulikia suala hiyo. Kwa hivyo, JSC imetupilia mbali malalamishi yao dhidi ya Jaji Isaac Lenaola,” JSC ikaambia wawakilishi wa Bi Naishorua, kampuni ya mawakili ya Murgor & Murgor Advocates.

Malalamishi mawili dhidi ya Jaji Mabeya yaliyowasilishwa na Bw Havi na Bw Dande, pia yalikataliwa.

Bw Havi alipinga uamuzi uliotolewa na Jaji Mabeya katika kesi kuhusu mzozo wa ardhi kati ya Kamati ya Msikiti wa Pumwani Riyadha na Kampuni ya Gikomba Business Limited.

JSC ilisema japo malalamishi hayo yaliafiki matakwa hitajika, rufaa imewasilishwa dhidi ya uamuzi kuhusu kesi hiyo na Mahakama ya Rufaa imetoa uamuzi wake.

“Kwa mtazamo wa tume, kushughulikia malalamishi kama hayo kutakuwa sawa na kubatilisha uamuzi wa mahakama, hatua ambayo iko nje ya mamlaka ya JSC,” Bi Mokaya akaeleza.