Habari

Mitaa na taasisi muhimu Nairobi zakosa maji

Na CHARLES WASONGA August 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

JUMLA ya mitaa 15 na taasisi muhimu jijini Nairobi zinakumbwa shida ya maji, kampuni ya huduma za maji na maji-taka ya Nairobi (NWSC) imethibitisha.

Kupitia ilani kwa wateja iliyotoa Jumapili, NWSC ilisema hali hiyo katika usambaji wa maji inachangiwa na hitilafu za kiufundi katika mabomba ya kusambaza maji kutoka Kabete-Kibera-Langata.

Hata hivyo, kampuni hiyo imesema mafundi wao wametumwa katika mitaa iliyoathiri kurekebisha hitilafu hiyo.

Mitaa ambayo wakati huu inaathirika na changamoto hiyo ni Lang’ata, Kibera, Kilimani, Lavington, Parklands, Westlands na Kileleshwa.

Aidha, mitaa iliyoko kando na barabara za Ngong’, Lang’ata na iliyoko kando ya barabara ya Raila Odinga, kama vile Madaraka, Nyayo Highrise, Nairobi West na Dam pia inaathirika na uhaba wa maji.

Taasisi zinazoathirika ni pamoja na; hospitali ya Nairobi Hospitali, Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Bewa Kuu la Chuo Kikuu cha Nairobi na bewa na Chiromo.

“Tunawashauri wateja wetu kutumia vizuri maji waliyohifadhi. Aidha, tumetuma magari yenye matangi ya maji katika mitaaa inayoathirika na tatizo hili ili wakazi wachote maji bila malipo,” ikaeleza ilani hiyo iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mkuu wa NWSC Nahashon Muguna.

Nairobi, yenye karibu wakazi milioni tano, hutumia lita 900 milioni ya maji kila siku.

Lakini wakati huu, NWSC husambaza lita milioni 525 kila siku, kiasi ambacho ni chini ya kiwango hitajika.

Kampuni hiyo haikutangaza ni lini hali ya kawaida ya usambazaji wa maji itarejelewa, lakini ikasema inaendelea kufuatilia hali huku ikitoa njia mbadala za kuhakikisha wakazi wanapata bidhaa hiyo muhimu.