Mshtuko polisi wakimuua karani wa zamani wa kaunti ‘kimakosa’
ALIYEKUWA Karani wa Bunge la Kaunti ya Siaya Isaac Olwero jana aliuawa kwenye baa anayomiliki katika eneo la South West Seme, Kaunti ya Kisumu.
Mauaji hayo yanadaiwa kufanyika kimakosa kwa kuwa meneja wa baa hiyo alikuwa amepiga ripoti kuhusu uvamizi huo na kuitisha msaada wa maafisa wa usalama.
Ripoti ya polisi ilisema kuwa maafisa hao walikuwa wakipiga doria kabla ya kupokea simu kuwa baa hiyo ilikuwa imevamiwa.
“Naibu chifu alipata habari kutoka kwa meneja kuwa wezi walikuwa wakivunja lango la kuingia kwenye baa. Pia aliwaita maafisa wa polisi kutoka Kombewa ambao walikuwa wakishika doria,” ikasema ripoti katika kituo cha polisi cha Kombewa.
Katika kupambana na wezi hao, ripoti ya polisi ilisema mmoja wa maafisa alimpiga kimakosa mmiliki wa baa hiyo ambaye alikuwa amejificha kwenye kichaka na akafa papo hapo.
Mauti ya Bw Olwero yanakuja wakati ambapo amekuwa akisaka haki kortini mara kwa mara akidai alifutwa kazi kama karani bila sheria kufuatwa.
Mwanaharakati wa haki za kijamii Chris Owala amesema mauti hayo si ya kawaida na yanastahili kuchunguzwa na Idara ya Upelelezi Nchini (DCI).
“Ameuawa wakati ambapo alikuwa akipanga kukata rufaa kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Uajiri na Leba Kisumu wa kutupilia mbali kesi yake. Mauaji yake si ya kawaida na yanastahili kuchunguzwa,” akasema Bw Owala.
Katika kesi yake ambayo ilifutiliwa mbali na Jaji Nzioki wa Makau, Bw Olwero alitaka arejeshwe kazini na pia alipwe fidia ya miezi 12 kwa kufutwa kazi kinyume cha sheria.
Bw Olwero alitimuliwa afisini mnamo 2019 kutokana na madai ya ufisadi na licha ya mahakama kuamrisha arudi kazini, hakuruhusiwa kukanyaga afisi yake.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo mnamo 2022, alidai alifurushwa afisini na watu ambao walikuwa na nia ya kupora pesa za Kaunti ya Siaya.
“Nilisimamia uwazi katika matumizi ya fedha na sheria na hiyo iliwakasirisha baadhi ya watu kwenye uongozi wa Bunge la Kaunti. Hata baada ya mahakama kuamrisha nirejee kazini, uongozi walinizuia kuingia afisini,” akasema Bw Olwero mnamo 2022.