Habari za Kitaifa

Rigathi kutikisa jiji, kuhutubia umma Kamukunji akirudi Alhamisi

Na CECIL ODONGO, MWANGI MUIRURI August 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha DCP kimeonya serikali dhidi ya kuvuruga kurejea kwa aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, huku ikisema mwanasiasa huyo atawahutubia wafuasi wake katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi mnamo Alhamisi.

DCP jana iliwataka Wakenya wajitokeze kwa wingi kumlaki Bw Gachagua akitua katika uwanja wa Jomo Kenyatta baada ya kuwa Amerika kwa ziara ya mwezi mmoja.

“Tunataka kuwatangazia kuwa ratiba ya kurejea kwa Bw Gachagua haijabadilika na kiongozi wetu atakuwa akitua nchini Alhamisi hii baada ya ziara ya mmwezi moja Amerika,” akasema Naibu Kiongozi wa DCP, Cleophas Malala.

“Msafara utatoka uwanja wa JKIA saa mbili asubuhi hadi katikati mwa jiji na baadaye Gachagua atafululiza hadi uwanja wa Kamkunji – sehemu ya historia ya nchi ambako atahutubia mkutano wa hadhara,” akaongeza Bw Malala.

Alidai kuwa wamemfahamisha Inspekta Jenerali wa Polisi kuhusu shughuli hizo na kutoa wito wapewe usalama wa kutosha.

Iwapo serikali itamzuia Bw Gachagua JKIA, Bw Malala amewataka wafuasi wake wajiandae kumpokea katika uwanja wa ndege wa Kisumu au ule wa Mombasa.

Aidha, alitoa onyo kuhusu jaribio lolote la kumkamata aliyekuwa naibu rais akisema hakutakuwa na utulivu jinsi ambavyo ilikuwa alipotimuliwa mnamo Oktoba mwaka jana.

Anaporejea Bw Gachagua anasubiriwa na changamoto kadhaa za kisiasa katika jitihada zake za kumng’oa madarakani Rais William Ruto mnamo 2027.

Mwanzo anarudi wakati ambapo kumekuwa na wito kwamba anyakwe kutokana na madai aliyoyatoa akiwa Amerika kuhusu serikali na matamshi tata ya kuharibia utawala huu jina.

Aliyekuwa naibu rais alidai kuwa utawala wa Rais Ruto unashirikiana na magaidi kutoka Somalia na pia unahusika na ukosefu wa uthabiti Sudan kwa kushirikiana na wapiganaji wa RSF.

Kati ya wanaomtaka Bw Gachagua anyakwe ni Msaidizi wa kibinafsi wa Rais Ruto, Bw Farouk Kibet.

Hata hivyo, Bw Malala ametishia kuwa ‘mbingu itashuka’ iwapo Bw Gachagua atanyakwa katika uwanja wa ndege akirejea nchini.

Pia Bw Gachagua anarejea kupata upinzani ambao umelegea na kunywa maji huku makali yaliyoonekana akiwa nchini yakikosekana.

Badala ya mikutano ya kisiasa Viongozi wa Upinzani – Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Eugene Wamalwa, Justin Muturi miongoni mwa wengine – wamekuwa wakishiriki tu vikao na matamshi yao yamekosa kutikisa serikali ya Ruto.

Pia moto unawaka ndani ya DAP-K kati ya Bw Wamalwa na Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, kila mmoja akionekana kulengwa kuwa kiongozi wa chama hicho.

Bw Natembeya hata ametishia kuondoka DAP-K iwapo hakutakuwa na demokrasia ndani ya chama hicho.

Katika uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini itabidi Bw Gachagua ajikune kichwa iwapo atawachia DP au DCP itakuwa na mwaniaji.

Bw Muturi ambaye ni kiongozi wa DP amependekeza Diwani wa Muminji ambaye pia ni mwanamuziki Newton Karish aungwe mkono na upinzani.

Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku ambaye alikiacha kiti hicho alichaguliwa mbunge wa eneo hilo 2022 kwa tikiti ya DP.

Kwa upande mwingine DCP nayo inataka kumwasilisha Diwani wa Evuvore Duncan Mbui kuwania kiti hicho.

Pia kuna makundi mbalimbali ambayo yamejitokeza kupambania ubabe wa Mlima Kenya na itabidi aliyekuwa naibu rais apambane na hilo ili aendelee kudumisha ubabe wake wa kisiasa eneo hilo.