Harambee Stars waogelea dimbwi la mamilioni huku wakielekeza jicho kwa Madagascar
BAADA ya kushinda mechi zake zote za Kundi A katika Kombe la Afrika kwa Wachezaji Wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024), Harambee Stars sasa itaelekeza nguvu zake zote katika kushinda mechi ya robo fainali dhidi ya Madagascar Ijumaa hii.
Haya yanakuja wakati ambapo wanasoka wa Harambee Stars wanaendelea kufurahia mamilioni kutoka kwa serikali. Pesa za hivi punde ambapo wanasoka hao wamepewa ni Sh3 milioni kwa kila mchezaji kwa kuishinda Zambia 1-0 mnamo Jumapili.
“Nashukuru Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa kutimiza ahadi na pesa zote zimelipwa kwa wachezaji. Sasa tunaangazia mechi ya robo fainali mnamo Ijumaa,” Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Hussein Mohamed akaambia Taifa Leo baada ya kuungana na Waziri wa Michezo Salim Mvurya kuwapa wanasoka hao pesa hizo.
Rais Ruto alikuwa ameahidi kila mchezaji atalipwa Sh2.5 milioni huku Odinga akiongeza Sh500,000 kwa kila mchezaji na kutoa tangazo hilo viongozi hao walipokutana na wachezaji wa Harambee Stars ugani Kasarani baada ya ushindi dhidi ya Zambia.
Tangu dimba lianze kila mchezaji na benchi ya kiufundi wa Harambee Stars amepokea Sh6.5 milioni.
Walishinda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) na Morocco ambapo kila mchezaji alilipwa Sh1.5 milioni kwa kila ushindi, kisha sare dhidi ya Angola ilimvunia kila mwanasoka Sh500,000 na Sh3 milioni katika ushindi dhidi ya Zambia.
Kuhusu mechi dhidi ya Madagascar, Kocha wa Harambee Stars Benni McCarthy amewataka vijana wake wajitume na kuishinda ili wawe na nafasi ya kutinga nusu fainali na hata kucheza fainali nyumbani.