Maoni

MAONI: Kindiki, Musalia wasipoleta viti vya Mbeere na Malava nyadhifa zao zitwaliwe na ODM

Na CECIL ODONGO August 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais Prof Kithure Kindiki na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi wanastahili kuhakikisha UDA inashinda Malava na Mbeere Kaskazini, la sivyo nafasi wanazoshikilia zipewe wandani wa Raila Odinga ifikapo 2027.

Kati ya chaguzi zote sita za maeneo bunge ambazo zitaandaliwa mnamo Novemba mwaka huu, Malava na Mbeere Kaskazini ndizo zitakuwa na mtihani mkubwa.

Mwanzo, Prof Kindiki na Bw Mudavadi hawafai kushikilia nafasi walizo nazo bila kura, ilhali wandani wa Raila ambao wamehimili serikali wamepewa nyadhifa serikalini.

Kiti cha eneobunge la Mbeere Kaskazini kilikuwa kikishikiliwa na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, ambaye aliwania kupitia chama cha DP mnamo 2022.

Tunu aliyopewa ya kuwa waziri baada ya Justin Muturi, ambaye pia anatoka eneo hilo, inafaa kuambatana na kiti hicho kuendea UDA.

Ushindi wa UDA katika Mbeere Kaskazini utaonyesha kuwa Rais William Ruto bado ana kura za maana eneo hilo, hata kama si nyingi ikilinganishwa na kabla ya uchaguzi mkuu uliopita.

Hii ndiyo maana Bw Ruku na Prof Kindiki wanastahili kushughulikia kwa makini Mbeere Kaskazini na kuhakikisha UDA inashinda.

Iwapo mrengo unaoegemea aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua utashinda Mbeere Kaskazini, basi Rais Ruto asahau kura za Mlima Kenya 2027.

Hiyo ina maana kuwa Prof Kindiki pia atapoteza wadhifa wake, kwa sababu jamii nyingine haziwezi kumpigia kura Rais kisha faida iende kwa mrengo ambao haujamuunga mkono.

Mbeere Kaskazini iko Mlima Kenya Mashariki, ambayo ni himaya ya Prof Kindiki kama ilivyo Tharaka-Nithi na Meru. Kwa hivyo, akaze buti na ahakikishe UDA inashinda eneo hilo iwapo anataka kubaki na nafasi yake.

Eneo la Malava, Bw Mudavadi lazima ahakikishe mrithi wa Malulu Injendi anatoka UDA.

Bw Mudavadi ndiye mwanasiasa serikalini anayenufaika na matunda ya uongozi bila kuleta kura zozote za maana.

Katika uchaguzi uliopita, hata Kaunti ya Vihiga anakotoka ilimpigia Raila Odinga kura.

Isitoshe, mbunge wa sasa wa Vihiga ni wa UDA licha ya kwamba mnamo 2022 Bw. Mudavadi alimsimamisha mgombea wa ANC, chama ambacho kilivunjwa mwaka jana na kujiunga na UDA.

Enzi za Bw. Mudavadi kufurahia mazuri ya serikali bila kuleta kura zimepitwa na wakati. Anapaswa kuhakikisha UDA inashinda Malava.

Iwapo Bw Mudavadi na Prof Kindiki watashindwa kuhakikisha UDA inapata viti hivyo, basi wajipange kupokezwa makombo 2027.

Kwa sasa, kuna kila ishara kuwa Bw Odinga na wafuasi wake wanamuunga mkono Rais Ruto kuchaguliwa tena 2027.

Iwapo ataleta kura nyingi na Rais Ruto ashinde, basi yeye atapewa wadhifa wa Waziri Mkuu na wafuasi wake wajazwe serikalini.

Rais Ruto naye amejaribu kuvutia vijana kupitia miradi na mechi za Harambee Stars, baada ya kuanza kupoteza uungwaji wao.

Iwapo Prof Kindiki na Bw. Mudavadi hawataleta chochote mezani, basi viti vikubwa vitawatoka.

Kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka aliwahi kuondolewa kwenye mahesabu ya UhuRuto kwa sababu kura zake zilikuwa chache na alikataa kupokezwa wadhifa wa Spika wa Bunge la Kitaifa.

Bw Mudavadi na Prof Kindiki wasishtuke iwapo kura zitawalemea, bali wakubali nafasi ndogo.

Iwapo wataona hilo halifai, basi Kenya ni nchi ya kidemokrasia na wanaweza kuchukua mwelekeo mwingine wa kisiasa wanaoupenda.