Maoni

MAONI: Katika madai yote ya Gachagua dhidi ya Ruto, la muhimu ni kile Amerika inafikiria

Na DOUGLAS MUTUA August 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KABLA hujashangilia au kukashifu vitisho vya kumkamata Naibu wa Rais aliyetimuliwa, Bw Rigathi Gachagua, vinavyotolewa na serikali ya Kenya, kwanza jiulize: Kati ya Bw Gachagua na Rais William Ruto, Amerika inamsikiliza nani?

Serikali ya Kenya imetishia kumkamata na kumhoji Bw Gachagua kutokana na hotuba zake kali alizotoa katika ziara Amerika, hasa madai kuwa Dkt Ruto ana ukuruba na wahalifu wa kimataifa.

Inasemekana madai yaliyoiudhi serikali ya Kenya ni yale ambapo Bw Gachagua alisema Rais Ruto hivi majuzi alikutana na viongozi wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab na anawaunga mkono waasi wa Sudan, Rapid Support Forces (RSF).

Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw Kipchumba Murkomen, alisema kwa hasira kuwa serikali itamkamata Bw Gachagua mara tu akirejea nchini ili aeleze ni kina nani hao aliodai wanamfichulia siri za serikali.

Kwa sasa, jipe hamnazo kwamba Bw Murkomen hakuyakanusha madai yenyewe; lake kuu lilikuwa kujua yalikoanzia.

Basi, huenda Bw Gachagua analipa kisasi cha kisiasa. Yana umuhimu na athari gani katika uhusiano wa Kenya na Amerika?

Ikizingatiwa kuwa Amerika imetumia mabilioni ya Dola katika vita dhidi ya magaidi, hasa Al-Shabaab, itahisije ikijua kuwa Kenya, mshirika wake wa tangu jadi, huenda anatoboa mashimo kwenye dau la mapambano hayo?

Lipo swali jingine muhimu la kujiuliza unapotafakari haya: Katika mgogoro wa Sudan ambapo majeshi ya kitaifa yanapigana na waasi wa RSF, Amerika inamuunga mkono nani?

Ukipata majibu ya maswali hayo, itakuwa rahisi kuelewa kinachoendelea, labda hata uelewe jukumu ambalo Dkt Ruto anatekeleza katika misukosuko hiyo miwili.

Kumbuka, Kenya si taifa la kawaida; ni mshirika mkuu wa Amerika katika eneo la Maziwa Makuu, na kiongozi wake anatunza maslahi ya Amerika kwa kiasi kikubwa.

Si siri kwamba mataifa mengi ya Afrika huiona Kenya kama mtu wa mkono wa Amerika.

Wakati huu ambapo taifa hilo tajiri zaidi duniani linaongozwa na Donald Trump, mtu mwenye sifa za ajabu zisizofanana na za mtangulizi wake yeyote, mambo yanafanywa tofauti kabisa na yanavyotarajiwa.

Huenda umeketi hapo ukijiambia Dkt Ruto amechafuliwa jina machoni pa jamii ya kimataifa, kumbe walimtuma wao kujaribu kuwaelewa magaidi wa Al-Shabaab na waasi wa RSF!

Labda sisi, na hata Bw Gachagua, tunachezewa mchezo wa kimataifa.

Hiyo ni mbinu inayotumiwa sana kuitawala dunia.

Hata mataifa hasimu zaidi, hasa wakati wa migogoro, huwa na njia fiche za kuwasiliana, mara nyingi kupitia washirika wenye ujuzi na nafasi ya kipekee ya kupatanisha wagombanao.

Mathalan, kwa mara kadhaa ambapo Amerika imewahi kushambulia Iran na maslahi yake kijeshi, Iran, kupitia kwa washirika kama hao, imeitumia Amerika ilani ya kulipiza kisasi na kubainisha kisasi chenyewe kitakuwa na uzito gani, tena kwa muda gani.

Juzi tu, Rais Trump amekutana nchini Amerika na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, ambaye ametukanana naye kwa miezi kadhaa, kumbe kisiri wamekuwa wakipanga kikao cha kujadili vita vya Ukraine na hali ilivyo barani Ulaya!

Kikawaida, inapohusiana na kiongozi wa nchi yoyote, Amerika huangalia maslahi yake kwanza, si ubora au umaarufu wa kiongozi husika nchini mwake.

Ni kwa sababu hiyo ambapo dikteta wa Rwanda, Paul Kagame, juzi amepewa mkataba wa kuwapokea na kuwatunza wahamiaji haramu wanaofukuzwa Amerika, hata ikiwa si Wanyarwanda.

Ni kwa sababu za maslahi ya Amerika ambapo inaendelea kushirikiana na serikali dhalimu ya Saudi Arabia, ambayo huhukumu watu kifo katika hali za kutatanisha na kuwaua kinyama bila kukumbushwa kuhusu umuhimu wa haki za binadamu.

Ikiwa Amerika ilimtuma Dkt Ruto kukutana na Al-Shabaab, au ilimpa idhini ya kuwaruhusu waasi wa RSF kuundia serikali mbadala ya Sudan jijini Nairobi, basi wengine sote, hata tukilalamikaje, tunasaga meno tu.

Swali la kujiuliza ni rahisi: Amerika inasemaje?

mutua_muema@yahoo.com