Makala

Ulemavu umemnyima mengi, ikiwemo penzi la dhati ila anajivunia hatua alizopiga

Na JURGEN NAMBEKA August 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 5

MNAMO 1976, wakati ambapo waokoaji walikuwa wakijaribu kuokoa abiria na miili kutoka kwenye gari moshi lililokuwa limepata ajali eneo la Kathekani, Kaunti ya Makueni, mtoto mmoja alikuwa akipambania maisha yake katika hospitali huko Mombasa.

Nafisa Khanbai, alikuwa amezaliwa na tatizo la uti wa mgongo, na alihitaji upasuaji wa dharura.

Huku madaktari wengi wakishughulikia majeruhi wa ajali hiyo, ni mmoja tu aliyekuwepo kutekeleza upasuaji huo.

Babake alitoa ruhusa ya upasuaji, licha ya kujua kuwa kulikuwa na hatari ya upande wa juu au chini wa mwili wake kufeli kutokana na upasuaji.

Katika kesi ya Nafisa, sehemu ya chini ya mwili iliathirika, ila siyo kikamilifu. Na alianza maisha yake akiwa na ‘plasta’ ya kurekebisha miguu.

Karibu miongo mitano baadaye, Nafisa anajisukuma kwenye kiti cha magurudumu hadi kwenye Jukwaa katika eneo la maonyesho ya sanaa ya Swahili Pot akiwa na nguvu.

Anacheka, akisakata densi katika eneo hilo linalojulikana eneo la Mombasa, kuandaa michezo ya kuigiza, akitoa uongozi kwa wasanii wake, na akipata nafasi ya kuzungumza na Taifa Leo, wakati wa mazoezi.

“Maisha yangu yalianza na changamoto nyingi, ila pia wazazi wangu hawakuona ulemavu kama suala kubwa. Licha ya unyanyapaa kuwepo, familia yangu ilichagua imani,” akasema Nafisa mwenye tabasamu.

Kwa mujibu wake, wazazi wake waliendelea kutafuta matibabu ya hali yake akiwa mchanga. Safari za nchi za ng’ambo zilikatizwa baada ya madaktari nchini Uingereza kuonya kuwa chokora chokora za uti wa mgongo zingeleta shida zaidi.

Baada ya kurejea nchini alijiunga na shule ya Alibhai Panju ambayo kwa sasa inaitwa Jaffery Academy, ambako alikuwa mtoto wa pekee mlemavu.

Kundi zima la waigizaji wa mchezo wa ‘Unbroken Wings’ wakati wa mazoezi na mahojiano na Taifa Leo kwenye ukumbi wa maonyesho ya Swahilipot Julai 10, 2025. Picha|Jurgen Nambeka

Licha ya walimu kumshughulikia kwa upendo, wanafunzi wenzake hawakujua njia ya kuishi naye. Mara nyingi alitengwa wakati wa shughuli na michezo nje ya darasa na mwishowe akaamua kuacha shule baada ya kumaliza darasa la nane.

“Niliamua kumaliza darasa la nane kwa kuwa familia ilikuwa imejitolea kwa ajili yangu. Sikuenda shule ya upili. Nilianza kupata hedhi na miaka sita na kufikia miaka tisa figo zangu zote zikafeli. Nikafanyiwa upasuaji mwingine ulionifanya mtoto wa kwanza wa nchini kuekea mfuko wa kusaidia kupitisha mkojo,” akasema Nafisa.

Aidha, baada ya kuacha shule, Nafisa hakuacha kutafuta elimu mbadala. Alijiunga na masomo ya kusimamia shughuli za nyumbani, na hapo ndipo alianza kupata zawadi kwa ubunifu wake, na hata akajifunza kuzungumza Kiingereza kwa ufasaha.

“Nilipofika miaka 18 nilipata kazi yangu ya kwanza katika Hospitali ya kushughulikia watu waliopooza ubongo eneo la Tudor kaunti ya Mombasa. Nilikuwa nikilipwa Sh3,000. Nilijihisi vizuri sana na kumpatia babangu mshahara wangu wa kwanza,” akasema Nafisa.

Ila anaeleza kuwa kufanya huko kazi kulibadilisha mtazamo wake wa maisha.

“Mwanzoni nilidhani, ingekuwa suala gumu sana kwangu, kuwashughulikia watu wenye ulemavu mkubwa. Niliona watoto wenye ulemavu mkubwa zaidi. Hawakuwa hata na uwezo wa kujilisha. Na hapo mtazamo wangu ukabadilika, nikaacha kujihurumia,” akasema Nafisa.

Kwa mujibu wake, aligundua kuwa alikuwa na uwezo wa kufanya mengi bila kupewa usaidizi.

Isitoshe nafasi ya kusafiri kuelekea Afrika Kusini kama mwakilishi wa klabu ya Rotaract ilimsukuma hata zaidi. Alijipata akilala kwa nyumba za watu ambao hakuwajua na alishughulikia afya yake akiwa mbali na nyumbani.

“Hiyo safari ndiyo ilinifufua na kuniwezesha kuanza safari ya kujivumbua upya, ilinionyesha nguvu zangu,” akasema.

Baadaye, alianza kushinda tuzo, kujiunga na mashirika, kufanya miradi ya kijamii na kuwa mmoja wa waanzilishi wa Shirika la Dear Diary, iliyoanza kama mchezo wa kuagiza mnamo 2006.

Kwa sasa imekuwa jukwaa la kutetea haki kupitia kuandaa michezo ya kuigiza nchini.

Katika juhudi za kuzungumzia matatizo ya walemavu nchini, Nafisa aliandaa mchezo wa kuigiza kwa jina “Unbroken Wings” uliofanyika mwezi Julai.

Mchezo huo uliohudhuriwa na zaidi ya watu 300, ulieleza hadithi ya Neema, mwanamke mlemavu, aliyekuwa akipambania na maisha ya kila siku  kutoka kwa mahusiano hadi matatizo ya kikazi.

Kwa mujibu wa mwigizaji Magdalene Gathoni, anayeigiza kama Neema, mchezo huo ulionyeza changamoto za kimya kimya, unyanyapaa na vizingiti visivyoonekana ambavyo walemavu hupitia haswa katika mapenzi na kazi, huku wakionyesha ukakamavu.

“Neema anampenda mtu flani, ila mtu huyo hamwoni yeye kama mke kwa kuwa ana ulemavu. Tulilenga kuwapa changamoto Wakenya kuwa walemavu wanaweza kupenda, kuoa, na hata kuwa na familia. Ni zaidi ya takwimu,” akasema Bi Gathoni.

Nafisa ambaye anasema mchezo huo ulitokana na kitabu chake chenye kichwa sawa na hicho, anaeleza jinsi maisha yake yanajitokeza kwenye mchezo huo.

“Saa zingine sisi walemavu tunapitia mazito. Unaniona nikitabasamu ila hujui siku nilizoshindwa kulala, ni machozi. Kuna mtu alikuja maishani mwangu kama rafiki. Nikawa nimejua hatuwezi kupendana kwa kuwa mimi ni mlemavu. Yeye akasisitiza hadi nikamkubalia. Nilishtuka miaka minane kwenye mahusiano nikiambiwa na rafiki yake kuwa alikuwa amempata mchumba mwingine waliyefunga ndoa naye. Sisi pia ni binadamu na tunahitaji kupendwa,” akasema Nafisa.

Bi Gathoni, anaeleza kuigiza kwenye mchezo huo kulimpa changamoto sana kuhusu walemavu.

“Nilienda nyumbani huku mikono yangu ikiuma kwa kutumia kiti cha magurudumu. Kwangu ilikuwa tu uigizaji ila ninawaza jinsi ambavyo kuna mtu anapaswa kutumia chombo hicho maishani. Hilo lilinifanya nikanyenyekea sana,” akasema Bi Gathoni.

Msanii Martin Simiyu Mutinda, aliyeigiza kama rafiki ya Neema kwenye mchezo huo anaeleza jinsi mchezo huo ulimfungua macho. Bw Mutinda anaeleza kuwa kabla ya mchezo huo, hakujali wala kujua jinsi ya kutumia kiti cha magurudumu.

Mwigizaji Magdalene Gathoni wakati wa mawasilisho ya maigizo ya mchezo wa kuigiza ‘Unbroken Wings’. Picha|Jurgen Nambeka

“Nilihisi vibaya sana. Eti nimeishi maisha yangu yote bila kujua kutumia kiti hiki. Nilidhani ni kusukuma tu, kumbe kuna mengi,” akasema Bw Mutinda.

Bw Mutinda anaeleza kuwa kupitia kwa muziki, mchezo ulionyesha jinsi walemavu pia walikuwa na talanta na walipaswa kupewa nafasi zaidi katika majaribio ya kuwateua wasanii kufanya shughuli mbalimbali.

Mwigizaji mwingine, Michael Micheni, mwandishi wa michezo ya kuigiza aliyeigiza kwenye mchezo huo, anasema aliigiza kama John, ambaye alikuwa akimtupia kejeli kila mara Neema kwa hali yake ya ulemavu.

“John analeta sauti ya watu walio sawa na mtazamo wao potovu kwa walemavu. Anasema mambo ambayo watu huogopa kusema mbele ya walemavu. Mchezo ulinifundisha kuwa walemavu wanaishi na mazito ambayo sikuwahi kuwazia kabla,” akasema Bw Micheni.

Kwa mujibu wa Mwelekezi wa mchezo Bw Denis Mutiso, alitatizika sana baada ya kupokea mchezo na kugundua kuwa Neema alipaswa kuwa kwenye kiti cha magurudumu kuanzia mwanzo hadi Mwisho wa mchezo.

“Ilinilazima kufanya utafiti wa kutosha ili nimuelekeze Neema jinsi ya kufanya mchezo huo. Gathoni hana ulemavu, ila hapa anapaswa kupika, na kuigiza mchezo mzima akiwa ameketi. Kazi nzito,” akasema Bw Mutiso, ambaye pia ni mcheshi wa watoto.

Nafisa anaeleza kuwa, mchezo huo unaoisha na Neema akijiua kwa sababu ya kutelekezwa na jamii, ulipaswa kuashiria changamoto za walemavu.

“Nilimwambia Gathoni sehemu ya kwanza ya mchezo utakuwa na furaha nyingi. Ila sehemu ya pili nikamwambia iwe na hisia nyingi ili tuguze mioyo ya watazamaji. Bila hivyo hatuwezi kuleta mabadiliko,”akasema Nafisa.

Kwa mujibu wake, kifo cha Neema kilitumika kama chombo muhimu kuelezea hadithi hiyo na kuonyesha mateso ya walemavu na wanapofikia mwisho baada ya msukumo wa maisha.

“Kuna kesi za ubakaji, unyanyasaji na kutelekezwa. Nilitaka waliokuwa kwenye hadhira kuketi na kujiuliza, Je sisi ni jamii jumuishi?” akasema.

Aliongeza kuwa, kuweka rampu na lifti kwenye majuma hakumaanishi chochote iwapo haitaambatana na kuwaelewa walemavu.

Kuna majumba mengi ya kibiashara Mombasa ambayo hayana vifaa kama viti vya magurudumu ya kielektroniki ya kuwasaidia walemavu kufanya shughuli pekee yao.

Anaeleza kuwa duka kuu la Nakumatt ambalo sasa lilifungwa, lilikuwa likizingatia sana mahitaji ya walemavu, kulikuwa na sehemu maalum ya kuegesha magari na hata viti vya magurudumu vya kielektroniki.

“Zuru tu majumba kadhaa hapa nchini na utaona. Wanunuzi wanapaswa kuja na viti vyao na vile ni ghali? Vitu hivyo vidogo vina uzito sana. Vikiwepo inamaanisha hata mimi naweza kuenda kufanya manunuzi nikiwa pekee yangu na kwa hadhi,” akasema.

Licha ya Sheria ya Walemavu kuwepo na mapendekezo ya kuwaadhibu wanaowabagua walemavu, Nafisa anaeleza hana haja na faini hizo, ila kubadilisha mawazo ya watu.

“Mimi sihitaji hiyo milioni moja. Ninataka mabadiliko. Nitawashtaki watu wangapi? Ni milioni ngapi zitatolewa kabala ya mabadiliko kupatikana? Ni lini tutaona watu wakiwaheshimu walemavu sio kwa sababu ya sheria, ila kwa sababu ya kujali,” akasema Nafisa.

Kutoka kuwapa changamoto hadhira kwa michezo yake ya kuigiza, safari ya Nafisa imekuwa moja ya kujivumbua, na kubadilisha maisha moja baada ya nyingine.

Leo Nafisa ana Shahada ya Uzamifu ya Heshima siyo tu kwa sababu ya sanaa yake, bali kwa mabadiliko anayochochea.