Akili Mali

AKILIMALI: Anatumia migomba ya ndizi kuunda ‘rasta’ za kina dada kusukia nywele

Na WYCLIFFE NYABERI August 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KARATASI za plastiki au nailoni zinazidi kuwa kero kuu katika mataifa mengi kutokana na athari zake kwenye mazingira.

Nchi nyingi ulimwenguni, Kenya ikiwemo zimepiga marufuku matumizi ya karatasi za plastiki zinazotumiwa mara moja ili kupunguza uchafuzi wa mazingira tunamoishi.

Katika Kaunti ya Nyamira, mjasiriamali mmoja amebuni njia moja inayoweza kupunguza matumizi ya plastiki hizi katika kitengo cha ulimbwende katika masuala ya usukaji wa nywele.

Aska Kerubo, ni mmoja wa waanzilishi wa kampuni ya Wefahson Banana Farmers Cooperative, iliyoasisiwa mwaka 2006.

Kampuni hii yenye makazi yake katika eneo la Getare, kando ya barabara kuu ya Kisii-Nyamira, husindika ndizi na kuziongezea thamani ili kuunda bidhaa kama vile mvinyo, unga wa kutengenezea uji, biskuti na bidhaa nyinginezo.

Lakini zaidi ya hayo, kuna upekee ambao umeiweka kampuni hii tofauti na zingine zinazosindika ndizi kuunda bidhaa sawia na hizo.

Upekee huo ni wa kuunda nywele bandia kutoka kwa migomba ya ndizi. Nywele hizo, hutumiwa na wasusi kurembesha kina dada au wanawake ambao ni wapenzi wa usukaji nywele.

Jarida la Akilimali lilipata fursa ya kumhoji Bi Kerubo kuhusu mchakato mzima unaohitajika kuunda nywele hizo.

“Tulipoanza kampuni hii mwaka 2006, tulikuwa tukisindika ndizi ili kuziongezea thamani. Tulikuwa tukisaga unga wa ndizi kuunda biskuti, mvinyo na vitu vingine. Lakini baada ya kusheheni ujuzi wa kutosha katika biashara hii, tuligundua kuwa migomba ya ndizi, ambayo mara nyingi tulikuwa tunaitupa au kuilisha mifugo, ni dhahabu ambayo inaweza kutuinua kiuchumi,” Bi Kerubo anasema.

Kulingana na mjasiriamali huyu, walifanya utafiti kuhusu namna ya kufanikisha hili na baada ya miaka michache, walianza safari hiyo.

Anaeleza kuwa shughuli ya kuunda nywele hizo maalum ni rahisi ikiwa una ujuzi wa kufanya hivyo.

Anasema kwamba, mgomba wa ndizi hukatwa kulingana na urefu wa nywele wanazozitaka. Ukishakatwa, mgomba huo husafishwa na kunyumbuliwa maganda yake.

Kwa kutumia vitana au vitu vyenye ncha kali, maganda ya mgomba huo hukwaruzwa kuondoa tishu nyororo.

Tishu nyororo zikishaondolewa, zinabaki zile ngumu ambazo huelekezwa katika mashine spesheli.

“Katika mashine hiyo, tishu au nyuzi hizo zilizonyumbuliwa hutibiwa kwa chumvi na bidhaa zingine ii kuzilainisha na kuzipa mvuto na rangi inayohitajika. Zikishaondolewa kwenye mashine, zinaruhusiwa kukauka kabla ya kupakiwa tayari kwenda sokoni,” Bi Kerubo anasema huku akiongeza kuwa shughuli ya kutengeneza nywele hizo maalum huchukua angalau siku tano.

Mfanyabiashara huyu anaongeza kuwa kiwango cha nywele hizo bandia wanazozitengeneza hutegemea na idadi ya wafanyakazi.

“Ikiwa wafanyakazi ni wengi, utatengeneza nywele nyingi bandia. Pia vile vile, ikiwa mtengenezaji anatumia mashine, huwezi kumlinganisha na mtu anayetumia mikono yake tu,” Bi Kerubo anaongeza.

Kuna manufaa mengi ya kutumia nywele za migomba ya ndizi kulingana na Bi Kerubo.

Mjasiriamali huyu anadokeza kuwa wateja wao hawalalamiki kuhusu ubora wa nywele hizo kwani hazina madhara yoyote katika vichwa vyao.

“Watu wengi mara nyingi hujikuna wanaposukwa na nywele za plastiki lakini hizi zetu, wateja ambao wamezijaribu wanasema hawajapata madhara yoyote kama vile kujikuna. Hii ni dhihirisho kuwa bidhaa zetu ni mojawapo ya zile bora katika safu ya ulimbwende,” anasema.

Pia mfanyabiashara huyu anahoji kuwa nywele zao hazichafui mazingira kama zile za plastiki.

“Ukishavuliwa nywele hizi kichwani mwako na kuzitupa shambani, za migomba ya ndizi huoza na kurutubisha udongo. Lakini zile zingine, haziozi miaka nenda miaka rudi na hili huchafua mazingira yetu,” anaongeza.

Mbali na kutengeneza nywele maalum, Bi Kerubo anahoji kuwa wao huunda bidhaa zingine kama vile vikapu, mikufu, vipuli na mazulia kutokana na migomba ya ndizi.

Ubunifu wa kampuni hii ya Wefahson Banana Farmers’ Cooperative si tu wa kujichumia riziki bali pia ni mfano bora wa uvumbuzi ambao unachangia katika utunzaji wa mazingira wakati ulimwengu unazidi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababishwa pakubwa na tabia za kibinadamu kama vile uchafuzi wa mazingira.

Mbali na soko la humu nchini, Bi Kerubo anaeleza kuwa wanalo soko kuu katika mataifa ya nchi za nje lakini hawatoshelezi mahitaji yake.

Ndio maana anatoa himizo kwa watu wengine hasa vikundi vya kina mama na vijana kuingilia ujasiriamali kama huu kwa kuwa unaweza kuwa njia nzuri ya kujiwezesha.

“Nina imani kuwa kina mama na vijana walio mashinani wakipata ujuzi kuhusu namna ya kutengeneza nywele bandia kama hizi, wanaweza kuyabadilisha maisha yao ikizingatiwa kuwa nafasi za ajira katika taifa letu zinazidi kuadimika kila kuchao,” analeza.

Katika kazi yoyote ile, hakukosi kuwa na changamoto. Mjasiriamali huyo anaeleza kuwa hawajapata msaada wa kutosha kutoka kwa serikali za kaunti au ile ya kitaifa katika kuwaimarisha zaidi.

“Ikiwa tunaweza kupata mitambo au mashine za kisasa, tunaweza kutengeneza nywele nyingi lakini kwa sasa, hatuna mashine za kutosha na inatubidi tufanye kulingana na uwezo wetu,” anaongeza.