Usithubutu kupeana ‘direct ticket’, wafuasi wa UDA Baringo waonya Kindiki
UDA imejipata kwenye mzozo mkali na wapigakura katika Kaunti ya Baringo kuhusu mfumo wa uteuzi wa mwaniaji wa kiti cha useneta kwenye uchaguzi mdogo wa Novemba 27.
Uongozi wa UDA kupitia Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki unataka wagombea wakubaliane ili mmoja wao apokezwe tikiti ya moja kwa moja.
Kwa upande mwingine, wafuasi wa chama hicho nao wanataka wapewe nafasi ya kuamua mgombeaji wa chama.
Kiti cha useneta Baringo kilisalia wazi kutokana na mauti ya William Cheptumo mnamo Februari 15 baada ya kuugua kwa muda.
Alhamisi wiki iliyopita, zaidi ya wajumbe 3,000 wa UDA walikutana na Profesa Kindiki nyumbani kwake mtaani Karen ambapo walizungumzia uchaguzi huo mdogo.
Wakati wa mkutano huo mtaani Karen, Profesa Kindiki alipendekeza kuwa zaidi ya wagombeaji 10 wanastahili kuelewana bila kushinikizwa ili mmoja wao awanie kiti hicho.
Iwapo hilo litakosekana basi itabidi waendee mchujo ambao unaonekana kutochangamkiwa sana na uongozi wa chama.
Kati ya wale ambao wanataka tikiti ya UDA ni madiwani wa zamani Sylas Tochim na Reuben Chepsongol wengine wakiwa Wycliffe Tobole, Vincent Chemitei, Lineus Kamket, Isaiah Kirukmet, Evans Mundulel, Daniel Kiptoo, Joseph Cherutoi na Isaac Chebon.
“Iwapo wawaniaji wenyewe watakutana na wakubaliane bila kushinikizwa basi binafsi nitawasilisha majina ya wale ambao wamesalia kwa Rais William Ruto ili watafutiwe nafasi serikalini. Lakini lazima wakubaliane wenyewe mwanzo,” akasema Profesa Kindiki.
“Mkikubaliana, tutaheshimu na kuwasitiri wale ambao hawatapata tikiti ya chama. Iwapo wawaniaji wanataka wasaidiwe na wazee basi wapo huru kufanya hivyo bila kuingiliwa na shinikizo za kisiasa,” akaongeza.
Naibu Rais alirudia matamshi hayo alipozuru Chemolingot, eneobunge la Tiaty mnamo Ijumaa na Marigat Jumamosi.
Alisisitiza kuwa iwapo wawaniaji hawatakubaliana, basi itabidi washiriki mchujo ambao utamridhisha kila mmoja wao.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Baringo nao wanasema makubaliano ambayo yanavumishwa na Profesa Kindiki yanalenga kuwafungia nje wawaniaji wengine.
“Hatutaki tulazimishiwe mwaniaji kwa sababu wapigakura lazima wachague nani watamchagua kupitia uteuzi huru na haki. Tunataka mtu ambaye ana maslahi ya watu rohoni wala tusilazimishiwe mwaniaji,” akasema Yassin Hamisi kutoka Kabarnet.
Bartunen Ruto kutoka Baringo Kusini naye alisema makubaliano yanakiuka demokrasia.
“Wale ambao wana mzaha ndio hunufaikia makubaliano. Wawaniaji wote wanafaa kushiriki mchujo na yule maarufu zaidi ashinde na kupeperusha bendera ya chama,” akasema.
Viongozi wa kieneo akiwemo Joshua Matetai nao walimlilia Rais William Ruto ahakikishe kuwa wawaniaji wote wanapewa nafasi ya kushiriki mchujo na atakayeibuka bora zaidi awahi ushindi.
“Watu wa Baringo lazima waruhusiwe wamchague kiongozi wanayemtaka bila kuingiliwa na wanasiasa pamoja watu wenye ushawishi mkubwa serikalini,” akasema Bw Matetai.