Habari

Walimu walio na digrii wazimwa kufundisha JSS

Na WINNIE ATIENO August 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAMIA ya walimu wa shule za msingi waliotuma maombi ya kuteuliwa kufunza katika shule za Sekondari ya Msingi (JSS) wamezuiwa kufuatia tangazo la Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) iliyoweka masharti mapya ya uajiri.

Kwa mujibu wa TSC, walimu waliohitimu na Digrii ya Elimu (Chaguo la Msingi) hawafai kufundisha wanafunzi wa JSS.

Kenya ina zaidi ya walimu wa msingi 220,000, wengi wakiwa na diploma au digrii, huku wachache wakiwa na uzamili au hata uzamifu.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Bi Everleen Mutei, alifichua kuwa, tume hiyo ilipokea jumla ya maombi 3,718 kutoka kwa walimu wa shule za msingi waliotaka kuhamishwa hadi JSS.

Hata hivyo, ni walimu 1,436 pekee waliohitimu kulingana na vigezo vilivyowekwa.

“Pamoja na waraka huu ni orodha ya walimu 1,436. Mara baada ya kupokea, mnahitajika kuwachambua upya na kuwahamisha walimu waliotimiza masharti kufunza JSS kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa,” alisema Bi Mutei.

Alisisitiza ni walimu waliohitimu kufundisha katika shule za upili pekee ndio wanaostahili kuhamishwa hadi JSS.

Katika waraka uliotumwa kwa wakurugenzi wa elimu wa maeneo na kaunti ndogo, TSC ilieleza kuwa walimu wenye Digrii ya Elimu (Chaguo la Msingi) hawatimizi masharti ya kufundisha JSS.