Habari

Ufisadi: Kikosi cha Ruto chazimwa hata kabla ya kuanza kazi

Na RICHARD MUNGUTI August 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA Kuu imezuia kwa muda utekelezaji wa agizo la Rais William Ruto la kuunda kikosi maalum cha mashirika mbalimbali kupambana na ufisadi, hadi kesi iliyowasilishwa kupinga hatua hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa.

Jaji Bahati Mwamuye alitoa agizo la muda kufuatia ombi la wanaharakati wanne wakiongozwa na Dkt Magare Gikenyi, wakidai kuwa agizo hilo la rais ni kinyume cha sheria, lisilo halali na linakiuka Katiba.

Agizo hilo linaahirisha utekelezaji wa ‘Agizo la Rais kuhusu kuundwa kwa kikosi cha mashirika mbalimbali kupambana na ufisadi’ lililotolewa Agosti 18, 2025. Hii inamaanisha kuwa kikosi hicho cha watu 11 kilichojumuisha maafisa wa serikali kutoka sekta za usalama na fedha hakitaruhusiwa kuendelea na kazi kama ilivyopangwa.

Jaji Mwamuye ameagiza kuwa kesi hiyo isikizwe na kuamuliwa ndani ya siku 90 kuanzia Septemba 9, 2025 tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Washitakiwa, akiwemo Mwanasheria Mkuu, EACC, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), na mashirika mengine ya serikali kama KRA na CBK wameagizwa kuwasilisha majibu yao kufikia Agosti 29.

Katika kesi yao, walalamishi wamedai kuwa Rais alivuka mipaka ya mamlaka yake kwa kuchukua kazi za Tume Huru ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), ambayo imepewa majukumu hayo na Katiba.

“Katiba haimpi Rais mamlaka ya kuunda chombo chochote cha kupambana na ufisadi,” wamesema katika kesi hiyo.

“Ukiangalia majukumu ya Rais kama yalivyoainishwa katika Kifungu cha 132(4) cha Katiba, ni wazi kwamba hana mamlaka ya kuunda chombo chochote cha kupambana na ufisadi. Mamlaka haya anayojipea hayapo katika Katiba yetu,” wanasema walalamishi.

Walalamishi wengine ni Eliud Matindi, Philemon Abuga na Dishon Keroti.

Wanaeleza kuwa pale ambapo Katiba imetoa majukumu mahususi kwa chombo fulani, Rais hana mamlaka ya kutekeleza majukumu hayo kwa niaba ya chombo hicho.

“Hii ina maana kuwa Rais hana uwezo wa kutekeleza majukumu ya tume huru ya Katiba kama vile EACC, kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 79 cha Katiba pamoja na Sehemu ya 11, 12 na 13 ya Sheria ya Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi ya mwaka 2011,” wanadai walalamishi.

Wanapinga uhalali wa Katiba wa agizo la Rais kwa jumla, wakisisitiza kuwa Rais alivunja vipengee vingi vya Katiba na sheria kwa kuunda kikosi hicho, kuchagua wanachama wake, kueleza malengo yake na muda wake wa kuhudumu.

Wanadai kuwa Rais alivunja Katiba kwa kuteua afisa kutoka ofisi yake kuwa mwenyekiti wa kikosi hicho, hali ambayo wanahisi inalenga kuzuia uchunguzi wa ofisi yake na kulinda masilahi binafsi.

Walalamishi pia walitaja ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambazo zimehusisha Ofisi ya Rais na madai ya ufisadi, kama vile ununuzi tata wa mfumo wa SHA kwa Sh104 bilioni na sakata ya ada ya E-citizen.

Wamesema kuwa kikosi hicho ni ‘nakala’ ya kazi ambazo tayari zinafanywa na mashirika ya kikatiba kama EACC na ODPP, hivyo kuwepo kwake ni matumizi mabaya ya fedha za umma.

Pia, wamepinga ushiriki wa mashirika kama CBK, KRA, na PPRA wakisema hatua hiyo inavunja dhana ya kutenganisha madaraka

Kwa upande mwingine, wamesema kuwa kuhusika kwa EACC kwenye kikosi hicho kunafanya tume hiyo isilinde mamlaka yake kama tume huru, na badala yake inaonyesha kuelekezwa na serikali kuu.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa rasmi Septemba 9, 2025, na inatarajiwa kuamuliwa kufikia Desemba 2025. Maamuzi ya mahakama yanaweza kuweka mwelekeo mpya kuhusu mipaka ya mamlaka ya rais katika vita dhidi ya ufisadi.UFU