Habari za Kitaifa

Nenda kaimbe ‘wantam’ kama unataka, aambiwa Samidoh barua ya kujiuzulu polisi ikikubaliwa

Na KAMORE MAINA August 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANAMUZIKI maarufu wa Mugithi, Samuel Muchoki almaarufu Samidoh, sasa yuko huru kujitosa kikamilifu katika muziki au hata kuwania wadhifa wa kisiasa, baada ya uongozi wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kukubali rasmi kujiuzulu kwake.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Taifa Leo, Samidoh alikoma kuwa afisa wa polisi wa Huduma ya Polisi wa Utawala (AP) kuanzia Julai 20, 2025.

“Tulipokea barua yake ya kujiuzulu na sasa yuko huru kufanya mambo anayopenda,” alisema Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alipoongea na Taifa Leo Jumatano.

Hatua hii inamaliza uhusiano wa muda mrefu wa utata kati ya Samidoh na idara ya polisi, hasa baada ya video moja kusambaa mtandaoni ikimuonyesha akiwa jukwaani akiimba huku umati ukipiga kelele za “wantam”, neno linaloashiria upinzani dhidi ya muhula wa pili wa Rais William Ruto.

Tukio hilo liliwakasirisha wakuu wa polisi, ambao walidai kuwa Samidoh alikuwa anajihusisha kisiasa kinyume cha kanuni za Huduma ya Polisi ambazo zinawataka maafisa kuwa waaminifu kwa serikali na kutoshiriki siasa.

Kufuatia sakata hiyo, Samidoh alihamishwa kutoka kikosi cha kawaida cha polisi hadi Kitengo cha Kukabiliana na Wizi wa Mifugo (ASTU) kilicho Gilgil.

Aidha, alikabiliwa na tuhuma za kutoroka kazi, hali iliyowafanya wakuu wake kuanzisha uchunguzi wa kinidhamu.

Ili kujiepusha na hatua hizo, Samidoh alielekea Mahakama Kuu mwezi uliopita akiomba dhamana ya dharura kuzuia kukamatwa kwake.

Mahakama ilikubali ombi hilo ikisema kwamba kibali cha kukamatwa kwake kilikuwa kimetolewa kwa misingi ya kisiasa.

Samidoh alidai kuwa madai ya kutoweka kazini yalikuwa njama ya kumwadhibu kwa misimamo yake ya kisiasa na kukosoa serikali.

Kwa mujibu wa taratibu za kinidhamu, kama uchunguzi ungempata na hatia, angeweza kupewa onyo, kutozwa faini au kufutwa kazi. Hata hivyo, kwa kujiuzulu, Samidoh alizuia mchakato huo kuendelea.

Ingawa alikaidi kupokea simu za waandishi wa Taifa Leo Jumatano, barua rasmi aliyoonyesha kortini Mei 20 ilionyesha kwamba alipewa ruhusa kusafiri Amerika kati ya Mei 20 hadi Juni 9, 2025.

Barua hiyo ilikuwa imesainiwa na Naibu Msaidizi Mkuu wa Inspekta Jenerali wa Polisi, Mathew Kutoh.

Kwa sasa, Samidoh anarudi kwenye ulingo wa muziki akiwa huru na huenda pia akaanza safari ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.