Habari za Kitaifa

Uongozi wa Bunge na Mahakama kukutana kujadili masuala tata

Na BENSON MATHEKA August 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

VIONGOZI wa Bunge leo wanatarajiwa kukutana katika mkutano wa tatu wa kujadili masuala ya uongozi utakaofanyika jijini Mombasa, kwa lengo la kutathmini utendakazi wa Bunge na kuimarisha ushirikiano na Idara ya Mahakama.

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, ataongoza mkutano huo ambao umepewa kaulimbiu: “Kufufua Ushirikiano na Maelewano ya Uongozi Kutekeleza Majukumu ya Bunge kwa Uwajibikaji.”

Katika siku ya kwanza, wajumbe watatathmini maendeleo yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu ya Bunge kama yalivyoainishwa kwenye Katiba. Aidha, watapitia azimio na mapendekezo yaliyotolewa katika mkutano sawia uliofanyika Januari mwaka huu.

Akihutubia Bunge Jumanne, Spika Wetang’ula aliwahimiza wabunge kulinda heshima na uadilifu wa taasisi hiyo, hasa wakati huu ambapo Bunge limekuwa likikabiliwa na ukosoaji kutoka kwa umma.

“Uadilifu wetu haunabudi kuwa wa hali ya juu isiyotiliwa shaka. Tunapaswa kuwa kama mke wa Kaisari ambaye hakuna mtu aliyethubutu kumtilia shaka,” alisema wakati wa kikao cha alasiri. Ijumaa, mkutano huo utaendelea kwa kikao cha pamoja kati ya uongozi wa Bunge na Idara ya Mahakama.

Spika Wetang’ula alithibitisha kuwa watafanya mkutano na Jaji Mkuu na Rais wa Mahakama ya Juu zaidi kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano huku wakiheshimu uhuru wa kila taasisi kwa mujibu wa Katiba.

“Tutakuwa na kikao cha wazi na Mahakama ili kuchambua uhusiano wetu, kuangalia ukweli wa mambo, na kuulizana maswali magumu,” alisema Spika Wetang’ula.Bunge ndilo hutenga bajeti kwa Mahakama na kutunga sheria zinazoathiri moja kwa moja utendakazi wa Idara hiyo.