Murkomen aapa kuiga Michuki katika vita dhidi ya wahalifu
WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, Jumanne aliapa kuiga msimamo thabiti wa marehemu John Michuki katika kupambana na uhalifu, utovu wa nidhamu na ufisadi katika sekta ya usalama nchini.
Akizungumza akiwa Kaunti ya Murang’a, Murkomen alitangaza kuwa serikali itawafungulia mashtaka ya ugaidi waandamanaji wanaozua ghasia, wakiharibu mali ya umma, miundomsingi, biashara na kuvamia afisi za serikali.
“Kwa heshima ya Michuki, sitaruhusu magenge na makundi yenye itikadi kali kueneza hofu. Kiongozi yeyote wa usalama anayefumbia macho makundi kama haya atachukuliwa hatua kali za kinidhamu,” alionya.
Waziri huyo alizungumza baada ya kukutana na maafisa wa usalama ofisini mwa Kamishna wa Kaunti, kabla ya kukagua shughuli za usajili wa vitambulisho katika Huduma Centre.
Baadaye, alihutubia kikao cha umma kilichowaleta pamoja wananchi, viongozi wa kisiasa, maafisa wa usalama na wasimamizi wa serikali katika baraza la mji.
Murkomen alisisitiza kwamba maandalizi ya uchaguzi wa 2027 hayawezi kufanikiwa iwapo hakutakuwa na amani na ushirikiano wa kitaifa.
Alitoa wito kwa wasimamizi wa serikali na maafisa wa usalama kuangazia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ishara ya utulivu.
“Mnaweza kuendelea kusema haya ni mashtaka ya kubuniwa lakini nani alisema? Unamwitaje mtu anayechoma mali ya umma au kuvamia kituo cha polisi?” alihoji.
Waziri Murkomen pia alibainisha kuwa anatekeleza agizo la Rais William Ruto la kupambana na ufisadi ndani ya idara za usalama.
“Ni lazima tukomeshe tabia ya idara zetu kutajwa kila mara katika orodha ya ufisadi. Wengine wanahusika moja kwa moja na pesa, lakini sisi bado tunaorodheshwa vibaya zaidi. Tunaweza kucheka, lakini hali hiyo ni ya kusikitisha,” alisema.
Kaunti ya Murang’a imeripotiwa kuwa na uhalifu unaoendeshwa na magenge ya vijana, yanayodhibiti sekta ya usafiri wa umma, machimbo ya mawe, vituo vya kutupa taka na mashamba makubwa.
Murkomen alitoa agizo kwa maafisa wa usalama na utawala kuboresha mawasiliano, akionya kuwa serikali haiwezi kuruhusu taswira yake kuharibiwa kwa sababu ya uzembe na ukosefu wa uwazi.
“Hadithi ya mafanikio ya serikali haiwezi kuachwa mikononi mwa wanasiasa pekee. Wasimamizi wa serikali ndio kiungo muhimu cha mshikamano wa taifa hili,” alisema.