Habari

Wabunge walipiza kisasi, waangusha mswada muhimu wa serikali

Na CHARLES WASONGA August 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SIKU moja baada ya Rais William Ruto kudai bunge ni ngome ya ufisadi, wabunge, kwa hasira wameanza kuonyesha kucha zao kwa kuangusha miswada na maamuzi ya kisera ya Serikali Kuu.

Jumanne, Kamati ya Usalama kuhusu Bunge ilitupilia mbali Mswada wa sheria mpya ya kuongoza shughuli ya kumpokeza mamlaka rais mpya baada ya uchaguzi.

Mswada huo uliodhaminiwa na Kiongozi wa Wengi, Kimani Ichung’wah unapendekeza Rais Mteule ateue mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Kusimamia Mpito wa Mamlaka ya Urais.

Aidha, mswada huo unapendekeza kuwa rais mteule ateue Katibu wa kamati hiyo ya wanachama 25, tisa kati yao wakiwa wawakilishi wake.

Mswada huo pia unapanua sheria hiyo ya kuongoza shughuli ya kumpokea rais mpya afisi ili kujumuisha maafisa wengine kama Mawaziri, Mwanasheria Mkuu na Makatibu wa Wizara.

Kulingana na sheria ya sasa, Rais aliye mamlakani ndiye huonekana kuwa na usemi mkubwa katika kamati hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma.

Lakini Kamati ya Bunge kuhusu Usalama inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo ilipinga mswada huo ikisema “sheria ya sasa inatosha”.