Michango ya ‘uwezeshaji’ ya Kenya Kwanza yagawanya viongozi Taita Taveta
MIKUTANO inayoendelezwa na wanasiasa wa mrengo wa Kenya Kwanza na wandani wao kuwawezesha wanawake katika sehemu mbalimbali za nchi, sasa imechochea mgawanyiko wa kisiasa katika Kaunti ya Taita Taveta.
Wanasiasa kadhaa wa eneo hilo wamekosoa shughuli hizo wakidai ni matumizi mabaya ya pesa za umma. Haya yanajiri baada ya baadhi ya wabunge waliochaguliwa kupitia upinzani kubadili misimamo yao na kujiunga na serikali.
Tayari michango hiyo imefanyika katika maeneobunge matatu kati ya manne katika kaunti hiyo yakiwemo Mwatate, Taveta na Voi.
Wanaopinga michango hiyo wamedai kuwa, ni mbinu za kisiasa za kujipatia umaarufu huku uchaguzi wa 2027 unapokaribia bila nia ya kusaidia wananchi ipasavyo.
Mbunge wa Wundanyi, Bw Danson Mwashako, alisema haoni faida yoyote kwa wananchi na akatilia shaka mahali fedha zinatolewa.
“Ni nani anaweza kutoa mamilioni kila mara? Mishahara yetu haiwezi kuturuhusu kutoa pesa kama hizo kila siku,” alisema.
“Walete pesa kwa watu wangu wa Wundanyi kwa sababu ni zetu, lakini sitaiunga mkono michango hiyo. Naunga mkono maendeleo ya maana pekee,” akaongeza, huku akiwahimiza wakazi kutofautisha kati ya misaada ya muda mfupi na maendeleo ya kweli.
Kwa upande mwingine, Mbunge wa Mwatate, Bw Peter Shake, ameunga mkono michango hiyo na kampeni ya kumchagua Rais William Ruto kwa muhula wa pili.
Hata hivyo, hivi majuzi alikumbana na upinzani mkali kutoka kwa wakazi wa Voi alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara.
Mbunge huyo alilazimika kukatiza hotuba yake baada ya kuzomewa na umati alipokuwa akipigia debe miradi ya serikali.
“Ni kweli naunga mkono kampeni ya muhula wa pili. Tumekuwa upinzani kwa muda mrefu bila faida. Tumeamua kuingia serikalini ili tupate maendeleo,” alisema.
Alitaja miradi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya na ujenzi wa masoko na nyumba za bei nafuu kama mafanikio ya serikali.
Mbunge huyo pia alidokeza kuwa anaweza kuondoka chama cha Jubilee ikiwa hakitamuunga mkono Rais Ruto katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“Wakiendelea kumpinga Rais, nitajiunga na chama kitakachosaidia watu wa Taita Taveta,” alisema.
Mbunge Mwakilishi wa Kike katika kaunti hiyo, Bi Lydia Haika, ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais, aliongoza mkutano wa uwezeshaji katika eneo la Voi na kutangaza kuwa atafanya mwingine Wundanyi.
“Hapo awali, tulichagua serikali lakini hatujawahi kuona maendeleo ya maana,” alisema.
Mbunge wa Voi Abdi Chome hakuhudhuria mkutano huo, huku akiendelea kushikilia msimamo wa upinzani.
Mbunge wa Taveta, Bw John Bwire, naye ameendelea kutetea uhusiano wake wa karibu na Rais Ruto, akisema yuko tayari kupoteza kiti chake 2027.
“Wengine wanasema nitakuwa mbunge wa muhula mmoja kwa kushirikiana na Rais. Lakini mafanikio ya kiongozi hupimwa kwa jinsi anavyobadilisha maisha ya watu wake, si muda anaokaa ofisini,” alisema.
Bw Bwire, Bw Mwashako na Bw Chome walichaguliwa kupitia tiketi ya Wiper.