Maswali yaibuka kuhusu vikao vya usalama vya Murkomen
MIKUTANO ya kitaifa ya Jukwaa la Usalama inayoendeshwa na Wizara ya Usalama wa Ndani chini ya usimamizi wa Waziri Kipchumba Murkomen imezua mjadala mkali nchini.
Ingawa mikutano hiyo inalenga kuhimiza majadiliano baina ya serikali na wananchi kuhusu masuala ya usalama, wachambuzi wa siasa na usalama wameanza kuhoji umuhimu wake halisi na matumizi ya rasilmali za umma.
Kwa mujibu wa Bw Murkomen, mikutano hiyo inalenga kuwa jukwaa la kitaifa la mazungumzo ya moja kwa moja kati ya raia na serikali kuhusu masuala ya usalama na ustawi wa jamii.
Anasema mikutano hiyo inalenga kutoa fursa kwa jamii kueleza wasiwasi wao, kutoa mapendekezo na kushiriki kutafuta suluhu za changamoto za kiusalama.
“Lengo letu ni kuhamisha jukumu la usalama kutoka juu hadi ushirikiano wa wananchi ili kila mmoja awe sehemu ya kuifanya Kenya kuwa salama,” alisema.
Hata hivyo, kuna hisia kwamba mikutano hiyo inamfaidi vyema Bw Murkomen kisiasa, ambapo anajijengea taswira ya kiongozi anayefanya kazi kwa bidii na anayesikiliza wananchi.
Lakini, mikutano hiyo pia imeibua masuala 10 makuu ambayo yanaweza kumjenga au kumuangusha Waziri huyo.
Mikutano hii imewezesha maafisa wote wa usalama wa kaunti kuketi pamoja na Waziri pamoja na wakuu wao kutoka Nairobi.
Mtaalamu wa Masuala ya wafanyakazi Bi Gladys Nduku, anasema kuwa jukwaa hili limevunja ukuta wa hofu ya mamlaka na kujenga hali ya usawa.
Hata hivyo, anasema kuwa ushirikishaji wa wananchi umekuwa dhaifu sana.
Kulingana na baadhi ya wachambuzi, Bw Murkomen anatumia fursa hii kuimarisha uungwaji mkono kwa Rais William Ruto kuelekea uchaguzi wa 2027 pamoja na kujijenga kisiasa binafsi.
Wakili wa Mahakama Kuu Bw Geoffrey Kahuthu, anasema kuwa ingawa kazi ya utumishi wa umma inamruhusu kutetea ajenda ya serikali, si halali kuingiza siasa za ushindani mbele ya maafisa ambao hawafai kuegemea upande wowote.
Naibu Kiongozi wa Chama cha Democracy for Citizens (DCP), Bw Cleophas Malala, alilalamikia kauli ya Bw Murkomen kuhusu Naibu Rais Rigathi Gachagua, akisema alidhalilisha hadhi ya afisi yake.
Migogoro ya jadi kati ya polisi na maafisa wa utawala haijatatuliwa kupitia mikutano hii. Bw Murkomen akiwa Murang’a alisema kuwa “maafisa wa utawala ndio wanaoaminika zaidi mashinani”, lakini kwa upande wa polisi hasa wa trafiki, aliwashutumu hadharani kwa kuchukua hongo waziwazi.
Katika Kaunti ya Laikipia, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nyahururu Bw Isaac Kimutus alizua taharuki aliposema wanawake hawafai kuajiriwa kwa wingi katika idara ya polisi kwa kuwa hawawezi kuhimili kazi ngumu.
Kauli hiyo ilipingwa vikali, na Waziri Murkomen pamoja na Inspekta Jenerali walilazimika kuomba radhi.
Maafisa wengi wametumia mikutano hii kulalamikia mfumo wa uteuzi, uhamisho, na adhabu zisizo na haki.
Maafisa wamelalamika kuwa wanasiasa hutumia mamlaka yao kuingilia uchunguzi, kukamatwa na hata kuzuia kesi kufikishwa mahakamani.
Wameeleza kwamba wanasiasa wanaowaunga mkono huingilia kazi zao na hata kutoa vitisho kwa kutumia ushawishi wa kisiasa.
Wadau wengine wanasema mikutano hii imekuwa ya “kuonyesha tu” kwani wanaochaguliwa kuzungumza huwa wamepangwa mapema, na hufungwa midomo na uwepo wa wakuu.
“Ukijua utalipwa posho na unaongea mbele ya Waziri, utaongea ukweli gani?” aliuliza Bw Isaac Mungai, mwenyekiti wa New Gema.
Wafanyabiashara wametumia fursa hizi kupendekeza kuundwa kwa kamati ili washiriki kama wajumbe, na pia kutafuta nafasi za kukutana na Rais.
Sekta ya pombe na uchukuzi wa umma imekuwa mstari wa mbele. Bw Kabiru Kanene wa Rwathia Distributors alisema, “Wafanyabiashara lazima waunge mkono serikali ya sasa hatuwezi kuwa wapinzani.”
Wanasiasa wa upinzani wanaoegemea vuguvugu la Wantam wamekuwa wakisusia mikutano hiyo, wakisema haijumuishi sauti tofauti.
Hata hivyo, Seneta wa Kiambu Bw Karungo Thang’wa alihudhuria kikao na kupigia debe kauli mbiu ya Wantam, akitaka usawa wa usalama katika mikutano yote ya kisiasa.
Swali kuu sasa ni iwapo malalamishi yaliyotolewa yatashughulikiwa. Bw Murkomen alisema, “Mengine yatahitaji mashauriano katika baraza la mawaziri, bunge na idara ya bajeti.”
Lakini pia alionya maafisa dhidi ya kulalamika kupita kiasi, akisema, “Angalau mna kazi… hiyo ni heshima na mliahidi mtafanya kazi katika hali yoyote.”