Habari za Kitaifa

Bunge na mahakama zaahidi kushirikiana kwa heshima

Na BENSON MATHEKA August 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Bunge la Kitaifa na Idara ya Mahakama zimeahidi kushirikiana kwa karibu ili kukabiliana na changamoto zinazokumba utekelezaji wa majukumu yao, bila kuingilia uhuru wa kila moja

Katika mkutano wa kihistoria uliofanyika kwa mara ya kwanza jijini Mombasa, viongozi wa taasisi hizo mbili walisema kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa mihimili ya serikali kushirikiana ili kuimarisha utiifu kwa katiba na utoaji bora wa huduma kwa wananchi.

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, aliutaja mkutano huo kuwa wa kihistoria na muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya Bunge na Mahakama kwa manufaa ya taifa.

“Mkutano huu kati ya uongozi wa Bunge na ule wa Mahakama ni wa kihistoria na ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya mihimili hii miwili kwa ajili ya maslahi ya taifa,” alisema Spika Wetang’ula.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Martha Koome alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya mihimili hiyo ya serikali hautaathiri uhuru wa Mahakama, akieleza kuwa mashauriano yanawezekana bila kuingilia uhuru wa maamuzi ya Mahakama.

“Mahakama itaendelea kuwa huru katika kutoa maamuzi yake. Ushirikiano haupaswi kueleweka kama kuingilia uhuru wa Mahakama,” alieleza Jaji Mkuu Koome.

Aidha, Jaji Mkuu alitoa wito wa kuongezewa bajeti, akisema kuwa Mahakama ina jumla ya vituo 143 pekee vya mahakimu, na mpango wake ni kuwa na angalau mahakama moja katika kila eneo bunge.

Spika Wetang’ula aliahidi kwamba Bunge litaunga mkono juhudi za kuongeza bajeti ya Idara ya Mahakama ili kuwezesha utoaji wa huduma kwa ufanisi kote nchini.