Habari za Kitaifa

Zigo la madeni linavyoramba Chuo Kikuu cha Moi

Na  BARNABAS BII August 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Chuo Kikuu cha Moi kinakabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha yakiwemo madeni ya kihistoria ya zaidi ya miaka 10, gharama kubwa ya mishahara inayofikia Sh450 milioni kwa mwezi, wafanyakazi wazee wanaopokea mishahara mikubwa, pamoja na kupungua kwa wanafunzi.

Haya yanajiri huku usimamizi wa chuo hicho na chama cha wahadhiri UASU wakizozana kuhusu utekelezaji wa makubaliano ya pamoja ya mishahara na kutolipwa kwa ada za kisheria wanazokatwa wafanyakazi katika mishahara.Inakadiriwa kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo utachukua muda mrefu zaidi kutokana na changamoto za kifedha.

Alhamisi, kaimu makamu wa chansela Profesa Kiplagat Kotut, alifichua kuwa chuo kinakabiliwa na hali ngumu ya kifedha inayozuia utekelezaji wa vipengele vya kifedha katika makubaliano ya kurejea kazini ya Novemba 2024. Alilaumu UASU kwa kutumia mgomo kuhujumu shughuli za taasisi hiyo wakati wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaposajiliwa kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026.

“Tunaendesha shughuli zetu kwa hasara. Kuna madeni ya kihistoria, mzigo mkubwa wa mishahara wa Sh450 milioni kwa mwezi, na wafanyakazi wazee wanaopokea mishahara mikubwa, huku idadi ya wanafunzi ikipungua. Hali hii imefanya iwe vigumu kutekeleza vipengele vya kifedha vya makubaliano hayo,” alieleza Prof Kotut.

Aliongeza kuwa vipengele visivyo vya kifedha tayari vimetekelezwa, na kutaja hatua ya UASU kuitisha mgomo wakati wa kupokea wanafunzi kuwa ya kuhujumu taasisi.

Prof Kotut alisema kuwa serikali ilitoa Sh1.5 bilioni zilizotumika kulipa mishahara, na kwamba chuo kwa sasa hakipati mapato ya ndani kuendesha shughuli zake.