Habari za Kitaifa

Piganieni haki zenu zitambuliwe, wanawake wahimizwa

Na MORAA OBIRIA August 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Ifikapo mwaka wa 2055, wanawake na wasichana nchini Kenya wanapaswa kuishi katika jamii ambapo haki zao zinatambuliwa kikamilifu bila vizingiti vyovyote.

Huo ndio ulikuwa ujumbe katika kongamano la siku mbili la NXTHer Summit, lililoandaliwa na Nation Media Foundation jijini Nairobi, ambapo viongozi walieleza hatua zinazohitajika kufanikisha mustakabali wa wanawake waliowezeshwa katika miongo mitatu ijayo.

Kongamano hilo lililofanyika chini ya kauli mbiu “Kuvunja Vizingiti Miaka 30 Baadaye”, lilikutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani, Afrika Mashariki na Kenya.

Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa barani Afrika, Dkt Mazyanga Mazaba, alisema kwamba kuimarisha haki za wanawake si mashindano kati ya wanaume na wanawake, bali ni kusawazisha nguvu na kufungua uwezo kamili wa wanawake.

‘Mustakabali wa kijinsia unapaswa kutuondoa katika hali ya kutafuta tu kiti mezani, au hata kuwa na menu mezani, bali tubadili kabisa meza yenyewe,’ alisema.

Aliongeza kuwa katika miongo ijayo, vyombo vya habari havipaswi kuwa kioo tu cha jamii, bali chombo cha kusukuma mabadiliko. Alisisitiza kuwa simulizi hazipaswi kuonyesha tu maisha ya wanawake bali pia zitoe ajenda na kuathiri sera.

Dkt Mazaba alisisitiza kuwa wanaume na wavulana wanapaswa kuwa washirika katika kusukuma mbele haki na usawa wa kijinsia.

“Usaidizi niliopata kutoka kwa baba yangu ni sehemu ya sababu zinazonifanya leo nitajwe miongoni mwa wanawake waliotimiza mafanikio. Lazima tutambue wanaume kama washirika katika kubomoa mifumo ya ukandamizaji,” alisema.

Kuelekea mwaka wa 2055, alitoa taswira ya bara la Afrika ambapo wanawake watakuwa viongozi katika sekta za teknolojia ya kisasa kama Akili Unde(AI), uchumi wa kidijitali, filamu, mitindo, na utamaduni bila ubaguzi wa kidijitali au kutengwa kimfumo.

‘Safari iliyo mbele haitakuwa rahisi,’ alionya, akitaja changamoto kama upinzani wa kisiasa, ukosefu wa usawa wa kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi, na kutengwa katika matumizi ya teknolojia.

“Lakini wito wangu kwenu ni kuwa na ujasiri. Usisubiri mtu mwingine kuleta mabadiliko. Kuwa wa kuleta mabadiliko katika nafasi yako mwenyewe.”

Mkurugenzi Mkuu wa Family Planning 2030, Dkt Samukeliso Dube, aliunga mkono wito huo akisema kwamba ndoto ya miaka ijayo lazima ijengwe juu ya upatikanaji wa huduma na haki za uzazi kwa wote.

Ifikapo 2055, alisema, wanawake wanapaswa si tu kujua wapi pa kupata huduma hizo, bali pia kuwa na ujasiri na uhuru wa kufanya maamuzi yao binafsi kuhusu uzazi.

“Hiyo ndiyo taswira tunayotamani,” alieleza. “Lakini hatujafika bado. Tunaona mashambulizi dhidi ya haki za wanawake duniani kote, hasa kupitia harakati za kupinga haki na mikataba kama wa Geneva, ambapo baadhi ya mataifa yanakana wajibu wao wa kulinda afya ya wanawake. Kisha kuna kupungua kwa ufadhili wa wahisani, jambo linalozuia upatikanaji wa huduma badala.”

Alisema nchi nyingi za Afrika bado zinategemea sana misaada ya wahisani kugharamia bidhaa za upangaji uzazi badala ya kuziweka kwenye bajeti zao za kitaifa. Hili linadhoofisha uendelevu wa huduma hizo.

Afisa Mkuu wa Masuala ya Kampeni, Masoko na Ushirikiano katika Nation Media Group, Bi Monicah Ndung’u, alisema kuwa uwezeshaji halisi wa wanawake huja si tu kwa kuwapa jukwaa bali pia mamlaka ya kuchangia mazungumzo yanayowahusu moja kwa moja.