Macho kwa Strathmore Leos kutetea taji la Embu 7s
MABINGWA watetezi Strathmore Leos watakuwa miongoni mwa vivutio vikuu wakati macho yote yakielekezwa kwa duru ya nne ya Ligi ya Kitaifa ya Raga ya wachezaji saba kila upande uwanjani Njukiri, Embu leo na kesho.
Viongozi KCB wako Kundi A pamoja na Daystar Falcons, Mwamba na wenyeji Embu RFC. Kundi B litakutanisha Strathmore, Impala, Kabras Sugar na Kabete Stallions waliopandishwa ngazi kutoka daraja la pili.
Menengai Oilers ambao walifika fainali ya Christie Sevens watavaana na Nakuru RFC, Nondescripts na Mean Machine katika Kundi C. Machine wanarejea juu baada ya muda mrefu. Kundi D litaleta pamoja Kenya Harlequin, Catholic Monks, MMUST na Zetech Oaks.
Strathmore watawania kujikakamua zaidi baada ya kukosa fainali ya Christie 7s.
Katika ligi ya wanawake, daraja la juu linajumuisha washindi wa Prinsloo 7s na Christie 7s Mwamba watafukuzia mafanikio zaidi dhidi ya Quins, Impala na Northern Suburbs.
Daraja la pili liko na NYS Ladies, Ruck IT, Meru na Murang’a Trojans. Daraja la pili la wanaume litakuwa na jumla ya timu 20 zilizotiwa katika makundi matano.
Baada ya Embu 7s ligi hiyo itarejea Nairobi kwa duru ya Kabeberi Sevens mnamo Septemba 6-7 kabla ya kukamilika Septemba 13-14 na Dala Sevens mjini Kisumu.