Habari

Wito serikali itenge fedha zaidi kukabiliana na dhuluma za kijinsia

Na WINNIE ONYANDO August 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA ya kutetea haki za watoto wa kike sasa yanataka serikali kuu na zile za kaunti kutenga fedha zaidi kusaidia kupambana na visa vya dhuluma za kijinsia nchini.

Akizungumza Ijumaa katika wadi wa Nairobi South B katika mkutano uliolenga kuangazia nuru kuhusu dhuluma za kijinsia, Nyawira Wahito, Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za watoto wa kike nchini linalojulikanalo kama Women and Girls Resources Center alisema kuwa visa hivyo vimeongezeka nchini hivyo kuitaka serikali kuwekeza katika programu mbalimbali zinazojenga watoto hasa wa kike.

Kando na hayo, alisema kuwa kujitambua mapema na kujiendeleza kielimu ni nguzo muhimu zinazowasaidia wasichana kujiepusha na hatari za kudhulumiwa kijinsia na pia kuwa na maisha bora ya usoni.

Naye diwani wa Nairobi South, Bi Waithera Chege, alitoa wito kwa waathiriwa wote kuripoti visa kama hivyo katika asasi za usalama ili wahusika wachukuliwe hatua kisheria.

“Hatupaswi kufumbia macho visa hivi. Yeyote atakayepatikana akiwadhulumu watoto lazima akabiliwe vilivyo na sheria,” akasema Bi Waithera.

Kauli yake iliungwa mkono na Chifu wa Mariguini, Bi Christine Marete, ambaye alionya vikali wahusika akisema vitendo hivyo havitavumiliwa katika jamii.

Viongozi hao walitoa kauli hizo katika hafla ya kutoa misaada mbalimbali kwa watoto wa kike katika wadi ya Nairobi South.

Zaidi ya wasichana 400 walihudhuria hafla hiyo, ambapo walipata mafunzo ya kujitambua na kujilinda dhidi ya dhuluma wanapojitayarisha kurejea shuleni wiki ijayo.