Pambo

Kuandaa harusi kubwa haimaanishi ndoa itakuwa ya furaha, wahitaji ukomavu

Na  BENSON MATHEKA August 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA enzi hizi ambapo harusi nyingi huwa za kifahari lakini ndoa nyingi hazidumu, ni muhimu kwa vijana kujiuliza swali  nyeti: Je, ninaandaa harusi au ndoa?

Maandalizi ya ndoa hayahusu tu mavazi, mapochopocho, picha, au mapambo tu bali yanahusisha ukomavu wa akili, hisia na roho.

Kabla ya kula kiapo cha ndoa, fahamu  kuoa au kuolewa ni zaidi ya  harusi, ni uamuzi unaohitaji busara, maarifa, subira, na uelewa wa kina kuhusu maisha halisi ya watu wawili.

Wanasaikolojia wanakubaliana kuwa ndoa haipaswi kuwa kimbilio la kutoroka upweke au matatizo ya kihisia.

Dkt Carl Jung, mtaalamu wa saikolojia, asema  ikiwa hujajitambua, hujajielewa, au iwapo hujajifunza kushughulika na hisia zako binafsi, basi ndoa haitakuwa tiba  bali itakuwa kioo cha matatizo yako.

“Kabla hujaingia kwenye ndoa, jiulize: Nina busara ya kushughulikia matatizo? Nitajibu kwa hasira au kwa akili? Ninaweza kujifunza hekima ya kukimya badala ya kulalamika kwa kelele?” ashauri Jung.

Dkt John Gottman, mtaalamu mashuhuri wa mahusiano ya ndoa, alisema kupitia makala yake  ya utafiti kwamba “siri ya ndoa yenye mafanikio si kuepuka migogoro, bali ni jinsi wanandoa wanavyoshughulikia tofauti zao.”

Anasema kwamba hekima katika ndoa si kukosa kutofautiana, bali ni kujua jinsi ya kushughulikia changamoto kwa heshima, upole, na mawasiliano bora.

Kwa vijana wa kike, ashauri, wanafaa kufahamu kwamba sura na umbo huvutia, lakini busara huvutia moyo wa mwanaume kwa muda mrefu.

Kama unataka kuwa malkia wa kweli, jifunze kuzungumza kwa heshima, kushirikiana kwa hekima, na kujenga maono ya pamoja na mwenzi wako wa baadaye.

“Kama mke, uzuri wako wa nje humvutia mumeo, lakini ni hekima  yako inayomfanya aendelee kukuthamini.
Ustadi wako wa kupendeza huvutia macho yake, lakini ni akili yako inayomshawishi.

Kwa vijana wa kiume, tambua kwamba kuwa mume si “mwanaume wa nyumba” kwa sauti kubwa au pesa nyingi tu, bali ni kuwa kiongozi wa kihisia na kiakili, mwenye uwezo wa kushughulikia shinikizo za maisha bila kudhulumu au kukimbia,” asema Gottman katika makala yaliyochapishwa kwenye jarida la Psychology Today.

Kabla hujaoa mtu, asema, kwanza tambua jinsi anavyokasirika, anavyokabiliana na hasara, na anavyotenda anapochoshwa. Upendo unaoishi ni ule unaoambatana na busara, heshima, na uwezo wa kusamehe.

Gottman asema ikiwa unajiandaa kuoa au kuolewa, weka juhudi kubwa si tu kwenye mavazi au keki ya harusi, bali kwenye maandalizi ya ndani – kiakili, kihisia, na kiroho.

Jifunze kuwasiliana, kusamehe, kuomba msaada, na kujenga uaminifu.