Pambo

Athari za wazazi kunyima simu watoto wao

Na  BENSON MATHEKA August 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Huenda umewahi kusoma kwamba mitandao ya kijamii na matumizi ya teknolojia ya kidijitali yanaweza kuathiri vibaya ubongo wa binadamu. Swali ni: Tufanye nini  ili kukinga watoto?

Watu wengi hawajui kuwa kuna njia zilizothibitishwa kisayansi za kukabiliana na athari hizi mbaya za kiakili na kihisia zinazoletwa na maisha ya kidijitali yanayobadilika kwa kasi kubwa.

Wazazi wengi hawataki watoto wao wahisi wametengwa. Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa Chuo Kikuu cha Maryland, Amerika, vijana wanaweza kuhisi upweke wanaponyimwa simu zao.

 “Tunaelewa kuwa mitandao ya kijamii ina madhara yake. Lakini mara nyingi, tunapotwaa simu au kuwazuia watoto kutumia mitandao, tunawaingiza hofu, huzuni au kujitenga kabisa,” inasema ripoti hiyo.

Watafiti wanasema hali hii inawaweka wazazi katika hali ngumu. “Tunataka watoto wetu wafurahie manufaa ya mawasiliano ya mtandaoni – ikiwa ni pamoja na matumizi salama ya mitandao – lakini pia tunataka kuwalinda dhidi ya athari zinazoongezeka,” unaeleza utafiti huo.

 Watafiti walitambua kwamba wazazi wengi huhofia madhara kama vile:kupungua kwa uwezo wa kuzingatia, tabia za uraibu mtandaoni (ikiwemo kamari kwa vijana), kujilinganisha na wengine kwa njia isiyo salama, kutukanwa au kunyanyaswa mtandaoni, kuacha shughuli zenye manufaa kama mazoezi, kujifunza au mawasiliano halisi.

Hata hivyo, ripoti za watafiti zinaonyesha uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya juu ya mitandao ya kijamii na afya duni ya akili. Huenda hali duni ya afya ya akili ndiyo inayopelekea matumizi kupita kiasi ya mitandao.

Badala ya kuwa na hofu kupita kiasi kuhusu jinsi mitandao inavyowaathiri watoto, wazazi  wanaweza kuchukua hatua madhubuti za kuwalinda. Jambo muhimu ni kujenga uhusiano wa karibu na watoto, kuwauliza jinsi wanavyojisikia kuhusu maisha na masomo yao. Vijana wengi huogopa kuwasiliana na wazazi kwa hofu ya kuwakosea au kuwaangusha.

Utafiti uliofanywa  2023 na shirika la Rothwell, Amerika, unaonyesha kuwa uhusiano mzuri kati ya mzazi na mtoto hupunguza hatari za matatizo ya kiakili yanayohusiana na mitandao ya kijamii.

Watafiti wanasema wazazi wako na nafasi ya kuongoza, kuelekeza, na kujenga mazungumzo ya wazi na watoto kuhusu maisha ya kidijitali. Kwa kufanya hivyo, wanawasaidia sio tu kuishi kwa usalama, bali pia kwa furaha, hekima, na uwiano wa maisha halisi na mtandao.