Pambo

Misingi ya kuvunja ndoa za Kikristo, Kijamii, Kihindu na Kiislamu nchini Kenya

Na BENSON MATHEKA August 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Ingawa ndoa huonekana kama taasisi takatifu na ya kuvutia katika dini mbalimbali, mara nyingine hugeuka kuwa uwanja wa vita – vita ambapo mtu hulala na adui wake. Wakati mwingine, hali ya ndoa huwa ngumu kiasi cha kufikia uamuzi wa kuachana. Hatua hii ya kuvunja ndoa hujulikana kama talaka, na kuna sheria maalum zinazodhibiti mchakato mzima.

Ndoa za Kikristo

Ndoa za Kikristo ndizo maarufu zaidi nchini Kenya kwa sababu ya idadi kubwa ya Wakristo. Hufungwa kanisani na viongozi wa dini walioteuliwa rasmi. Kwa bahati mbaya, si kila ndoa huendelea kwa furaha, na baadhi huishia mahakamani kwa ajili ya talaka.

Kulingana na Sheria ya Ndoa ya mwaka 2015, kuna misingi mitano pekee ya kuvunja ndoa ya Kikristo:Uzinzi uliofanywa na mmoja wa wanandoa,ukatili wa kimwili au kiakili dhidi ya mwenzi au watoto, kutelekezwa kwa muda wa angalau miaka mitatu mfululizo kabla ya kuwasilisha ombi la talaka, ukatili wa kipekee au wa kupindukia, kuvunjika kwa ndoa kusikoweza kurekebishwa.

Ndoa za Kijamii

Ndoa hizi pia ni za kawaida kwa kuwa ni rahisi kuandaa. Hufungwa na msajili wa serikali. Kama ndoa nyingine, nazo hukumbwa na changamoto, na hivyo huweza kusababisha ombi la kutengana au kuvunjwa kabisa kwa ndoa.

Misingi ya kuomba talaka katika ndoa za kiraia ni, uzinzi, ukatili, uovu wa kupindukia,  kutelekezwa kwa miaka mitatu na kuvunjika kwa ndoa kusikoweza kurekebishwa

Ndoa za Kitamaduni

Ndoa hizi hufungwa kulingana na mila na desturi za jamii moja au zote mbili za wanandoa. Mara nyingi huambatana na malipo ya mahari kama ushahidi wa ndoa hiyo. Talaka katika ndoa hizi huanza kwa kupitia upatanisho wa kimila, na iwapo hautazaa matunda, kesi hupelekwa mahakamani.

Msingi wa talaka katika ndoa ya kitamaduni ni uzinzi, ukatili, kutelekezwa, uovu wa kupindukia, kuvunjika kwa ndoa na sababu nyingine yoyote halali kulingana na sheria za kimila za mlalamishi.

Ndoa za Kihindu

Hufanywa kulingana na mila na taratibu za dini ya Kihindu. Talaka hutolewa kwa njia ya ombi mahakamani. Misingi ya talaka ni:Kuvunjika kwa ndoa kusikoweza kurekebishwa, kutelekezwa kwa miaka mitatu, mmoja kuasi dini ya Kihindu, Mwenzai kufanya ubakaji, ushoga, au uzinzi, ukatil na uovu wa kupindukia

Ndoa za Kiislamu

Hufungwa na Kadhi, Sheikh au Imam, kwa kuzingatia sheria za Kiislamu. Tofauti na ndoa nyingine, vipengele vya Sheria ya Ndoa ya 2015 visivyolingana na sheria za Kiislamu havitumiki kwa Waislamu.

Talaka hutolewa na Kadhi, Sheikh au Imam, kisha nakala ya uamuzi hupelekwa kwa msajili wa ndoa.

Misingi ya kuvunjwa kwa ndoa ya Kiislamu ni: Ndoa  kutowahi kutekelezwa kimwili, wanandoa kuwa katika uhusiano wa damu bila kujua wakati wa kuoana, Katika ndoa ya mke mmoja, mmoja alikuwa tayari ameoa au kuolewa, mmoja hakutoa idhini ya ndoa kwa hiari, mmoja  kutohudhuria sherehe ya ndoa, mke kuwa na ujauzito ambao si wa mume, pasipo mume kujua na  mmoja kuwa  na matatizo ya akili yasiyojulikana wakati wa ndoa

Ni muhimu kwa mtu yeyote anayeingia au anayevunja ndoa kufahamu misingi hii ili kulinda haki zake. Sheria hizi husaidia kutatua migogoro ya ndoa kwa haki na kuwapa wahusika nafasi ya kuanza upya maisha yao kwa matumaini mapya.