Jamvi La Siasa

Kibaki na Raila walivyorarua Katiba ya 2010

Na  SAMWEL OWINO August 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS wa tatu wa Kenya hayati Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga walipuuza vipengele muhimu vya Katiba ambayo ilikusudiwa kuunda kaunti 14 pekee, na badala yake wakaongeza kaunti hizo hadi 47 wakitumia wilaya zilizokuwepo wakati huo.

Ufichuzi huu umetolewa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula katika mahojiano na Taifa Leo kuhusu miaka 15 tangu kupitishwa kwa Katiba ya 2010, ambapo alisema kuwa huu ni wakati mwafaka wa kuibadilisha.

Kwa mujibu wa Bw Wetang’ula, kwenye rasimu ya awali ya Bomas, Wakenya walikuwa wamekubaliana kuhusu maeneo 14 ya kiutawala.

Katika mpango huo, maeneo ya Magharibi, Nyanza na Kati yangegawanywa kila moja kuwa vitengo viwili, Bonde la Ufa na Mashariki kuwa vitatu kila moja, huku Pwani ikibaki kama eneo moja.

Nairobi ilikuwa imeorodheshwa kama eneo la kipekee kwa hivyo halingekuwa sehemu ya serikali ya ugatuzi wala serikali kuu, bali lingekuwa kitovu huru cha serikali ya kitaifa ambapo vitengo vingine vingeshughulikia masuala ya kitaifa.

“Huo ungekuwa mpango mzuri sana. Tungekuwa na mamlaka imara za kikanda, kisiasa na kiuchumi, ambazo zingefanya vizuri zaidi. Lakini tulianza kubishana na kutoaminiana. Hatimaye, kila Mbunge alitaka eneo lake la ubunge liwe kaunti. Hali ikawa ngumu kudhibiti,” alisema Bw Wetang’ula.

“Rais Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga walikubaliana kiholela kuwa kila wilaya ya mwaka 1992 ingepewa hadhi ya kuwa kaunti. Hivyo ndivyo tulivyopata kaunti 47,” aliongeza.

Bw Wetang’ula alisema kuwa hadi wakati wa uhuru, kulikuwa na wilaya 42, lakini Rais wa pili wa Kenya Daniel Moi akaongeza tano – Vihiga kutoka Kakamega, Bomet kutoka Kericho, Tharaka Nithi kutoka Meru, Makueni kutoka Machakos na nyingine moja kutoka eneo la Pwani.

“Hivyo ndivyo tulivyojikuta na kaunti zenye uchumi mkubwa na unaoendelea kama Kiambu na Narok, na zingine ndogo sana kama Isiolo na Lamu. Lakini sasa, kwa kuwa ziliundwa kwa mujibu wa Katiba mpya, mabadiliko ya mipaka au idadi yake yanahitaji kura ya maamuzi. Ikiwa Wakenya watakubaliana na hilo, siwezi kusema lakini mtazamo wangu ni kwamba tuna kaunti nyingi mno na zingine hazina uwezo wa kujiendesha,” alisema.

Spika huyo anakiri kuwa Kenya ina kaunti nyingi mno ambazo zinapaswa kuunganishwa au kuchunguzwa upya.

“Tuna kaunti nyingi mno kwa nchi ndogo kama Kenya. Ukiangalia nchi kama Canada, ambayo ina ukubwa wa karibu nusu ya Afrika, ina majimbo tisa pekee. Australia, ambayo ni bara yenyewe, ina maeneo sita pekee na yote ni imara, yenye uwezo wa kiuchumi na kisiasa,” alisema.

“Kenya tuna kaunti ambazo, isipokuwa kwa miujiza ya Mungu, haziwezi kujitegemea kwa muda mrefu,” aliongeza.

Seneta huyo wa zamani wa Bungoma alisema huu ni wakati muafaka wa kuwa na mjadala wa kweli kuhusu baadhi ya vipengele vya katiba, kwani miaka 15 inatosha kuelewa kinachofanya kazi na kisichofanya.

Bw Wetang’ula ambaye alihusika katika kuandika Katiba ya 2010 katika Bomas, alisema Kenya imepiga hatua kubwa tangu kupitishwa kwake.

Kuanzia kupanuliwa kwa Bunge na kutenganishwa na Ikulu, hadi mahakama huru na huduma ya polisi, hadi kuimarika kwa ushirikishaji wa umma katika uongozi na kuanzishwa kwa ugatuzi, Wetang’ula alisema Katiba hiyo imeiletea Kenya faida nyingi.

“Nilipoingia Bungeni mwaka wa 1992, Bunge lilikuwa idara ya Ikulu. Karani wa Bunge alikuwa afisa kutoka Ofisi ya Rais, na kila kitu kilichofanywa Bungeni kilidhibitiwa na Ikulu,” alisema.

Alieleza kuwa Katiba mpya ilikuwa mchakato mrefu na mgumu uliotokana na wito wa kutaka mageuzi, hadi mafanikio ya kuifanya Kenya kuwa nchi ya vyama vingi kutoka mfumo wa chama kimoja.

“Taasisinyingi zilihisi kubanwa na kunyimwa uhuru chini ya Serikali Kuu na zilihitaji uhuru wa kiutendaji. Enzi hizo hata Mahakama haikuwa huru; majaji waliteuliwa na Rais bila ushauri. Sasa ni tofauti. Polisi walikuwa idara ya Ofisi ya Rais; sasa ni taasisi huru,” alisema.

Kwa mujibu wa Spika, mafanikio ya kwanza ya Katiba ni kuunda mihimili mitatu ya serikali ambayo ni huru lakini inategemeana.

Pia alisema kuwa kabla ya Katiba mpya, mchakato wa bajeti ulikuwa siri kubwa ya Serikali Kuu na hakuna aliyethubutu kuuzungumzia hadharani, lakini sasa ni mchakato wa wazi kupitia Bunge.

“Ilibadilisha kabisa mfumo wa bajeti nchini. Bajeti ilikuwa siri kuu ya Serikali Kuu; watu walifutwa kazi kwa kuvuja siri za bajeti. Sasa bajeti inajadiliwa wazi wazi Bungeni,” alisema.

Kuhusu ugatuzi, Bw Wetang’ula alisema umewafanya wananchi waelewe uwepo wa serikali nje ya Nairobi.

“Watu walioko maeneo ya mbali walikuwa wakisikia tu kuhusu serikali. Kulikuwa na hadithi za watu kutoka Turkana au Mandera wakisema ‘sisi tunatoka Turkana tunaenda Kenya’ walipokuwa wakija Nairobi. Lakini sasa mambo yamebadilika. Tumepeleka mamlaka ya kifedha na kisheria kwa bunge za kaunti,” alisema.

Licha ya changamoto, Bw Wetang’ula alisema ugatuzi ndiyo msingi na uti wa mgongo wa mafanikio ya Katiba ya 2010.

Alisema pia kuwa kuingizwa kwa ushirikishaji wa umma katika kila uamuzi wa kikatiba ni hatua muhimu iliyorudisha mamlaka kwa wananchi.

Hata hivyo, alieleza kuwa baada ya miaka 15, bado hakuna sheria inayofafanua namna ushirikishaji wa umma unapaswa kufanywa.

“Hatujaweka sheria kuhusu ushirikishaji wa umma yaani kina chake, upeo wake, na athari zake kwa mchakato mwingine,” alisema.

Miongoni mwa maswali anayotaka yafafanuliwe ni iwapo ikiwa Bunge moja limefanya ushirikishaji wa umma, la pili linapaswa pia kufanya hivyo; iwapo maoni ya wananchi yanapaswa kushinda yale yaliyomo kwenye mswada; na kama ushirikishaji wa umma ni wa lazima kisheria.

Ingawa alisifu mafanikio ya Katiba mpya, Spika alisema kuna haja ya kufanya mabadiliko.

“Nchi nyingi zilizopitisha Katiba mpya, kama sisi, huipa miaka kama mitano na kuipitia tena. Kisha unaangalia ikiwa kuna vitu vya ziada vya kuondoa na maeneo yanayohitaji kuboreshwa,” alisema.