Mwanamke kusota jela miaka 25 kwa kulisha mpenziwe sumu mpaka akafa
MWANAMKE mmoja amehukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani kwa kosa la kumuua mpenzi wake kwa sumu miaka mitatu iliyopita baada ya kumpikia chakula kilichochanganywa na dawa ya kuua wadudu.
Benter Achieng alianza kutumikia kifungo chake wiki iliyopita baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya Benjamin Were, mhandisi msaidizi wa ujenzi wa barabara, ambaye alipata matatizo ya kiafya na kufariki usiku wa Julai 4–5, 2022, katika nyumba yao mjini Kakuma, Kaunti ya Turkana.
Mama huyo wa watoto watatu alihukumiwa na Jaji wa Mahakama Kuu Reuben Nyakundi baada ya ushahidi wa kisayansi kumhusisha moja kwa moja na tukio hilo.
Mtaalamu wa serikali alieleza mahakama kuwa mabaki ya chakula tumboni mwa Were yalionyesha kuwepo kwa dawa ya kuua wadudu. Dawa hiyo pia iligunduliwa katika nyama na wali vilivyookotwa na polisi.
Mtaalamu huyo, Richard Langat, alisema hakuna sumu nyingine iliyopatikana kwenye sampuli hizo., na akaeleza kuwa sumu hiyo ni kali na huua mara inapomezwa.
“Uzito wa kosa hili una vipengele viwili: kwanza, jinsi marehemu alivyolishwa sumu na mpenzi wake ambaye waliishi naye; na pili, madhara na ushiriki wa mshtakiwa. Sababu za nia, dhamira, na mazingira vinaashiria kuwepo kwa nia ovu, japo upande wa utetezi haukukubaliana na hilo,” alisema Jaji Nyakundi.
Jaji huyo alibaini kuwa hakuna ushahidi kuwa sumu hiyo iliingia mwilini kwa bahati mbaya kutoka mazingira ya nje, na hivyo akahitimisha kuwa Were alikufa kutokana na kitendo kisicho halali.
Katika utetezi wake, Achieng alisema walikuwa wamepokea wageni usiku huo kabla ya yeye kupika pilau kwa chakula cha jioni.
Alidai kuwa Were alijihudumia kinywaji kutoka kwenye friji.
Hata hivyo, mahakama ilitupilia mbali maelezo yake “Sioni sababu yoyote maalum au ya kipekee itakayoshawishi mahakama hii kumpa mshtakiwa adhabu isiyo ya kifungo. Kwa kosa hili, namhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka 25 gerezani. Kipindi alichokuwa rumande kitahesabiwa kuwa sehemu ya kifungo,” aliamua Jaji Nyakundi.