Jinsi pesa zilitumika kuendeleza mauaji ya itikadi kali huko Kwa Binzaro, Kilifi
WAPELELEZI wa mauaji ya ibada potovu ya kidini ya Kwa Binzaro, ambako miili tisa ilifukuliwa kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita, sasa wanafuatilia jinsi fedha zilitumwa baina ya washukiwa.
Hii ni baada ya madai kwamba pesa nyingi zilitumika kufadhili shughuli za kueneza itikadi kali za kidini na kusafirisha waathiriwa hadi vichakani walikofunga mpaka kufa.
Hati zilizowasilishwa katika Mahakama ya Malindi zinaonyesha kuwa, washukiwa waliokuwa wakichunguzwa walituma na kupokea fedha ili kufanikisha shughuli zao, ikiwemo kukodisha nyumba mjini Malindi.
Inaaminika kuwa, ni katika nyumba hizo ambako waumini walihifadhiwa kwa muda na kufundishwa itikadi kali kabla ya kusafirishwa hadi eneo la Chakama, Kaunti ya Kilifi.
Walipowasili huko, walifungiwa, kunyimwa chakula, na hatimaye kufa wakifuata mafundisho potovu yanayohusishwa na mhubiri Paul Mackenzie, ambaye yuko kizuizini kwa kuhusishwa na mauaji ya awali kama hayo Shakahola.
“Mpaka sasa, makaburi kadhaa ya kina kifupi yamepatikana katika eneo la Binzaro ambako Kahindi Kazungu Garama, Thomas Mukonwe, James Kahindi Kazungu na Sharleen Temba Anido walikuwa wameanzisha makazi na kuwalazimisha waumini kufunga na kuwafungia ndani ili kuwazuia kutoroka,” polisi walisema.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, wachunguzi waliomba kibali cha kupata rekodi za benki na M-Pesa za washukiwa ili kufuatilia jinsi fedha zilitumwa na kupokewa.
“Uchunguzi wetu umebaini kuwa washukiwa walitumia fedha kusukuma mbele mipango yao ya kikatili. Tumepata kibali cha kufuatilia akaunti zao na mchakato huu unahitaji muda,” polisi walisema wakiiomba mahakama kuongeza muda wa kuwazuilia kwa siku 30.
Maafisa pia wanafuatilia ushahidi wa kielektroniki, ambao wanaamini unaweza kufichua mienendo ya mawasiliano ya wahusika wa kuandaa ibada hiyo.
Simu za rununu, laini za mawasiliano ya simu na vifaa vya kuhifadhia data vilivyochukuliwa kutoka kwa washukiwa vimepelekwa kwa maabara ya Polisi wa Kupambana na Ugaidi (ATPU) kwa uchunguzi wa kina.
Ripoti zinazosubiriwa kutoka kwa uchunguzi huo zitabainisha wazi kuhusu mifumo ya mawasiliano iliyotumiwa, uratibu na maagizo ya kifedha yaliyowaunganisha viongozi wa dhehebu hilo.
“Kikosi cha uchunguzi kinategemea sana data za simu na ushahidi mwingine uliopo kwenye ushahidi huo. Mara tu simu zitakapochambuliwa, zitatoa maelezo mapya katika kesi hii,” polisi walisema mahakamani.
Matokeo ya awali yanadai kuwa, washukiwa Garama, Mukonwe, Kazungu na Anido walizunguka nchi nzima wakieneza mafundisho ya Mackenzie kuhusu mwisho wa dunia.
Imedaiwa kuwa, walishawishi wafuasi wa dhehebu la Good News International Ministries kuacha makazi yao na kufunga mpaka kufa kama njia ya hakika ya kukutana na Yesu.
Wapelelezi wanaamini baadhi ya wafuasi walihifadhiwa katika nyumba za kukodisha Malindi kabla ya kupelekwa Kwa Binzaro.
“Uchunguzi pia umebaini kuwa Garama na Anido walikodisha nyumba nyingine kadhaa Malindi walikowapokea waathiriwa kabla ya kuwasafirisha Binzaro kufunga hadi kufa. Nyumba hizi lazima zibainishwe, ziorodheshwe na wamiliki wao kuandikisha taarifa, jambo linalohitaji muda zaidi,” polisi waliongeza.
Kulingana na uchunguzi unaoendelea, familia nyingi nchini Kenya zimeripoti kupotea kwa jamaa zao, wengi wakisemekana kutoweka baada ya kufuata mafundisho ya wafuasi wa Mackenzie.