Habari za Kitaifa

Kitovu cha Ulaghai: Duale aungama SHA inaandamwa na utapeli wa kushtua

Na LEON LIDIGU August 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAMLAKA ya Afya ya Jamii (SHA) imegeuka kuwa jukwaa kubwa la ufisadi huku hospitali na vituo vya afya mbalimbali kote nchini vikiendelea kughushi stakabadhi za matibabu ili kupokea malipo ya mabilioni kutoka kwa serikali.

Waziri wa Afya Aden Duale jana aliungama kuwa SHA inaendelea kuandamwa na ufisadi mkubwa akifichua kuwa zaidi ya vituo 1,000 vya afya vimefungwa, baadhi vikilemazwa kutokana na ulaghai wa malipo.

Haya yanajiri wakati ambapo Wakenya wakiwemo watu walioajiriwa na serikali, wakilalamikia huduma mbovu chini ya SHA ambayo ilichukua mahala pa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF).

“Tumeona vituo vya afya vikivumbua mbinu mpya za kuhadaa mtandao wa malipo lakini wajuzi wetu waliobobea katika masuala ya kidijitali, hutambua ukora huo punde tu unapoanza,” akasema Bw Duale jana.

“Ukora huo unaweza kutambuliwa katika hatua yoyote ile nao mfumo tunaotumia wa akiliunde (AI) umetusaidia mno. Vituo 728 vimefungwa na vingine 301 kushushwa viwango na Baraza la Wahudumu wa Kimatibabu na Matabibu nchini (KMPDC),” akaongeza.

Mnamo Agosti 8, Bw Duale alichapisha notisi kwenye gazeti la serikali ambapo vituo 40 vya afya vilifungwa na SHA.

Jana Bw Duale alifichua kwamba zaidi ya vituo 45 vya afya pia vitafungwa kwa kushiriki ukora wa kuilaghai serikali hela zake.

Kwa mujibu wa Bw Duale, serikali imekataa kulipa Sh10.6 bilioni kwa vituo vya afya kutokana na stakabadhi zilizogunduliwa kuwa na ukora na vituo vyenyewe kukosa kutimiza masharti yanayohitajika.

“Baadhi ya wahudumu wa afya hufanya ulaghai huo wakijua. Malipo ya Sh3 bilioni nayo yanaangaliwa upya kutokana na ukosefu wa stakabadhi za kuhakikiwa pamoja na mengine ambayo yanahusu Sh2.1 bilioni,” akasema Bw Duale.

Mnamo Agosti pekee SHA inaangazia stakabadhi za malipo ambapo serikali imetakiwa kulipa vituo vya afya jumla ya Sh7.6 bilioni.

Bw Duale alifichua kuwa wamegundua ukora ambapo vituo vya afya hudanganya kuwa vimefanya idadi ya juu ya upasuaji kuliko kiwango kilichowekwa kwa kila mgonjwa.

“Kuwasilisha stakabadhi zenye maelezo ya uongo kuhusu mgonjwa ni kinyume cha sheria. Baadhi ya hospitali hudanganya kuwa wagonjwa walilazwa ilhali walitibiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani,” akasema waziri huyo wa Afya.

Hospitali ya Nabuala, Kaunti ya Bungoma ni kati ya zile ambazo zilipatikana kuwa zimedanganya kwa kutumia stakabadhi za uongo ili zilipwe na serikali.

Ilitoa stakabadhi ya kufanyia upasuaji (c-section) mwanamke mmoja aliyekuwa akijifungua, kwa siku mbili, ilhali hakukuwa na stakabadhi za kuthibitisha kujifungua kwake.

Mfanyakazi wa kituo cha afya cha Kotiende, Homa Bay naye alighushi stakabadhi za kliniki zilizoonyesha kuwa alifanya kazi mchana na usiku kwa siku kadhaa zikifuatana ilhali ni jambo ambalo haliwezekani.

Kituo cha kimatibabu cha Vebeneza, Nairobi, nacho kilighushi stakabadhi kuonyesha wagonjwa waliokuwa wakitibiwa na kuenda nyumbani, kama wale ambao walilazwa.

Pia kituo hicho kilizua shaka kwa kuwasilisha stakabadhi zilizoonyesha kuwa hata wafanyakazi wao walilazwa na kutibiwa huko.

Nazo stakabadhi za mama aliyejifungua salama Hospitali ya Jambo Jipya, Mtwapa zilionyesha alikuwa amefanyiwa upasuaji, jambo ambalo lilikuwa uongo.

Vituo kadhaa vya kimatibabu Mandera navyo viliungana na kushiriki utapeli wa kuwapokea wagonjwa 312.

Kinaya ni kuwa baadhi ya wagonjwa walilazwa kwenye vituo mbalimbali siku moja tena wakati sawa.

Vituo vilivyoungana kushiriki ukora huo ni Al Masry, Rhamu Dimtu, Balanga, Care Connect, Al Shamshi, Merti, Zamzam na Nibil.