Waislamu North Rift wataka Supkem ivunjwe sababu ya ibada duni ya Hija huko Mecca
BARAZA la Maimamu na Wahubiri wa Kenya (CIPK) linataka kuvunjiliwa mbali kwa Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya (SUPKEM) kutokana na madai ya kutoshughulikia vyema mahujaji wa Kenya wakati wa ibada ya Hija jijini Mecca, Saudi Arabia.
Mwenyekiti wa CIPK kanda ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa, Sheikh Abubakar Bini, alieleza kutamaushwa na hali mbaya inayokabili mahujaji licha yao kulipa pesa nyingi kugharamia mahitaji yao.
“SUPKEM imeshindwa kutekeleza majukumu yake. Waislamu wa Kenya ambao walisafiri kwenda Mecca baada ya kulipa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya nauli na mahitaji mengine walikabiliwa na mazingira magumu,” akasema Sheikh Bini.
Akihutubia wanahabari mjini Eldoret mnamo Alhamisi iliyopita, Sheikh Bini alisema kutokana na uongozi usiowajibika wa Supkem mahujaji wa Kenya walioenda Mecca waliwekwa mbali na ukumbi mkuu kutokana na mipango duni.
Sheikh Bini alisema licha ya Waislamu kulipa ada kwa mawakala inavyotakiwa waliishia kuteseka Mecca.
Kwa mujibu wa Sheikh Bini mahujaji kutoka Kenya walilazimika kukaa kilomita 17 kutoka eneo kuu na pia kunyimwa malazi shwari.
“Ni wazi kuna tatizo kubwa katika uongozi wa SUPKEM na sababu kuu inayotufanya tulalamike kama CIPK ni jinsi hajj ilivyoendeshwa. Mahujaji waliokwenda Mecca waliteseka sana ilhali walilipa kiasi kikubwa cha pesa kujikimu,” alieleza mwenyekiti wa CIPK Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Rashid Kiplagat.
Hata hivyo, mwenyekiti wa kitaifa wa Supkem Hassan Naado alikanusha shutuma hizo na kusihi waislamu kutoingiza siasa katika dini.
“Masuala ya kidini hayatatuliwi kisiasa. Hajj ni mila ya kidini si suala la kisiasa kujadiliwa kwa namna yoyote,” akasema Naado katika mahojiano ya awali.
Anataka uongozi wa Supkem kujiuzulu mara moja ili kutoa nafasi kwa maafisa wapya watakaoshughulikia vyema hija ya mwaka ujao.
Naye mwenyekiti wa CIPK Kaunti ya Uasin Gishu, Rashid Kiplagat alisikitika, kwamba Supkem imeshindwa inafanya mapendeleo kwa Waislamu matajiri badala ya kuwatendea Waislamu wote haki kwa misingi ya kidini sio mali.
Hata hivyo mwenyekiti wa kitaifa wa SUPKEM Hassan Naado amekanusha kuhusika katika mateso ya mahujaji na kuwataka waislamu kujizuia kutoa kauli za uchochezi na kuingiza siasa katika masuala ya kidini.
“Tunafaa kukumbuka kuwa masuala ya kidini hayatatuliwi kisiasa, hajji ni mila ya kidini na si suala la kisiasa la kujadiliwa kwa namna yoyote,” alisema Naado wakati wa mahojiano ya awali.