Habari

Rais wa LSK Faith Odhiambo ateuliwa jopo la kufidia wahanga wa maandamano

Na CHARLES WASONGA August 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto ameteua jopo la wataalamu 14 watakaoongoza mchakato wa utoaji fidia kwa waathiriwa kwa makabiliano kati ya raia na polisi nyakati za maandamano ya kupinga serikali.

Kupitia tangazo kwenye gazeti rasmi la serikali toleo la Jumanne Agosti 26, 2025, Dkt Ruto amemteua Rais wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Faith Odhiambo kama naibu mwenyekiti wa jopo hilo la wanachama 15 litakaloongozwa na mshauri wake kuhusu masuala ya kikatiba Profesa Makau Mutua.

Wanachama wengine ni; wakili Kennedy Ogeto, mkurugenzi mkuu wa shirika la Amnesty International, tawi la Kenya Houston Irungu, Dkt John Olukuru, Kasisi Kennedy Barasa Simiyu, Mwanasheria Dkt Duncan Ojwang’, Naini Lankas, Dkt Francis Muraya, Juliet Chepkemei, Pius Metto, Fatuma Kinsi Abass, na Raphael Anampiu.

“Jopo hilo litatekeleza agizo la kirais kwa kuweka mpango wa kutambua, kuthibitisha na kutoa fidia kwa waathiriwa wa machafuko yaliyokumba maandamano nchini,” Rais Ruto akaeleza akiongeza kuwa watakaofaidi ni waathiriwa wa tangu 2017 hadi Julai mwaka huu.

Ili kufanikisha utendakazi wa wanachama wa jopo hilo, Rais ameteua kikosi cha kiufundi kitakachoongozwa na Richard Barno akisaidiana na Dkt Duncan Okelo Ndeda.

Nao Bi Jerusha Mwaathime Michael na Dkt Raphael Ng’etich watahuhumu kama makatibu wa jopo hilo.

Jopo hilo linatarajiwa kukamilisha kazi yake ndani ya muda wa siku 120 kuanzia tarehe ya uteuzi rasmi ya wanachama wake. Hata hivyo, linaweza kuongezewa muda zaidi endapo halitakuwa limekamilisha kazi ndani ya muda huo.

Katika kutambua waathiriwa halisi, jopo la Profesa Mutua na Bi Odhiambo litatumia data kutoka kwa asasi za serikali kama vile Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA), Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNCHR), Shirika la Kitaifa la Polisi (NPS) na Wizara ya Afya, kabla ya kupendekeza kiwango cha fidia kwa waathiriwa.

Zaidi ya watu 100 wamekufa na wengine wengi kujeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji tangu mwaka jana.