Habari za Kitaifa

Siri ya kukuza matawi ya biashara kunavyohakishia kampuni faida

Na BENSON MATHEKA August 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Kampuni iliyoorodheshwa kwenye soko la hisa, HF Group, imetangaza ongezeko la asilimia 148 ya faida kabla ya kodi, ikipata kutoka Sh 283 milioni katika kipindi cha nusu ya mwaka 2024.

Matawi yote ya biashara ya kampuni hiyo yalirekodi ongezeko la faida.

Mapato halisi kutokana na riba yaliongezeka kwa asilimia 53, yakifikia Sh 2.04 bilioni kutoka Sh 1.33 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Afisa Mkuu Mtendaji wa HF Group, Robert Kibaara, alisema ufanisi huu mkubwa ni thibitisho la mafanikio ya mkakati wa mabadiliko ambao umeendelea kuchochea ukuaji katika matawi yote.

“Tutaendelea kujenga kampuni thabiti na imara inayowapa thamani endelevu wadau wetu,” alisema.

“Utendaji wetu mzuri ni ushahidi wazi wa mafanikio ya mkakati wetu wa mabadiliko na utofauti wa huduma, ambao unaendelea kuchochea ukuaji katika kampuni zetu tanzu. Tunaendelea kujitolea kujenga kundi imara na linalostahimili mabadiliko, ambalo linawapatia wadau thamani endelevu.”

Aidha, alikiri athari chanya za mafanikio ya Utoaji wa Haki za Hisa ambao ulitoa msukumo wa kuharakisha ukuaji wa biashara katika maeneo mahususi ya soko.

Bw Kibaara pia alisisitiza kuhusu msimamo thabiti wa kifedha wa kampuni hiyo, akisema kwamba kiwango cha ukwasi kimesalia imara katika asilimia 51.4, zaidi ya mara mbili ya kiwango cha chini kinachohitajika na mamlaka.

Uwiano wa mtaji wa msingi kwa mali zilizopimwa kwa hatari ulifunga katika asilimia 21.3, zaidi sana ya kiwango cha chini kinachotakiwa cha asilimia 10.5.

Kitengo cha benki cha kundi hilo kimepandishwa hadhi rasmi kuwa benki ya kiwango cha pili kuthibitisha ukuaji wa sehemu ya soko na msingi imara wa mtaji.

Hatua hii imejiri baada ya mkakati wa mafanikio wa utofauti wa huduma wa kundi hilo, hadi kuwa benki kamili ya huduma pamoja na huduma zilizopanuliwa za mali isiyohamishika na bima.

Kupandishwa kwa hadhi ni ishara ya imani kubwa ya soko kwa taasisi hiyo na thibitisho la uwezo wa kundi kuendelea kukua kwa muda mrefu.