Walimu wakuu wanavyoua ndoto ya elimu ya bure nchini kutoza wazazi ada haramu
UTAFITI mpya uliofanywa na Action Group Kenya (CIAG-K) umebaini kuwa ahadi ya serikali ya kutoa elimu bure na ya lazima nchini Kenya inakumbwa na changamoto kubwa zinazotokana na ufisadi, udanganyifu, na ukosefu wa uwajibikaji.
Utafiti huu uliotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili ya kifedha (2020 hadi 2022), unaonyesha kuwa wakuu wa shule wamebobea sana katika matumizi mabaya ya madaraka yao kwa kutoza wazazi ada haramu, kuhamisha fedha za umma kiholela, na kupuuza miongozo ya elimu.
Takriban shule tisa kati ya kumi za umma hutoza ada haramu za kujiunga, ambazo zinaanzia Sh500 hadi Sh25,000, jambo ambalo ni kinyume na miongozo ya Wizara ya Elimu, Katiba ya Kenya pamoja na Sheria ya Elimu Msingi inayohakikisha elimu bure na ya lazima kwa watoto wote.
Ada hizi haramu ni pamoja na ada za dawati, kabati, kodi ya vitabu, michango ya maendeleo, pamoja na ada za mitihani na shughuli za shule.
Aidha, utafiti huo umebaini kuwa karibu asilimia 68 ya shule hazina stakabadhi za kutosha za matumizi na mapato yao, huku asilimia 85 ya shule zikionyesha tofauti kubwa na ukosefu wa uwazi katika rekodi za kifedha.
Hii inaashiria udhaifu mkubwa katika usimamizi wa fedha za shule na hutoa mazingira mazuri kwa ufisadi kuenea.
Pia, utafiti umegundua uhamishaji wa fedha za umma kwenda kwa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Kenya (KESSHA), kikundi ambacho hajatambuliwa rasmi na serikali kama taasisi inayopaswa kupokea fedha za umma.
Shule kama Maranda High School na Moi Girls’ Kamusinga zimeripotiwa kuhamisha zaidi ya Sh1.7 milioni kwa KESSHA, wakati shule nyingine nyingi pia zimehusika katika uhamishaji huu haramu wa fedha.
Utafiti wa ziada uliofanywa na Elimu Bora Working Group (EBWG) umebainisha kuwa takriban asilimia 90 ya shule za umma hutoza ada haramu.
Ufisadi umekuwa ukihusisha si tu ukusanyaji wa ada haramu, bali pia unajumuisha kudumisha wanachama wa bodi za usimamizi wa shule, migongano ya maslahi katika ununuzi wa vifaa, na uhamisho wa fedha kwenda kwa vyama vya walimu kama KESSHA na KEPSHA.
Athari za ufisadi huu ni kubwa na zinagusa maisha ya watoto wengi nchini. Takriban asilimia 65 ya shule hutuma watoto nyumbani mara kwa mara wazazi wakikosa kulipa ada hizo haramu.
Hali hii inasababisha watoto wengi wa shule ya msingi kukaa nyumbani kwa sababu ya ada zisizolipwa, huku asilimia 45 ya wanafunzi wa kidato cha kwanza wakiwa hatarini kuacha shule kabisa. Hali hii inaleta hatari kubwa kwa mustakabali wa elimu nchini Kenya na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Wakati wanafunzi wamerudi shuleni kwa muhula wa tatu mwaka huu, changamoto za kifedha kwa familia nyingi na ucheleweshaji wa ruzuku za serikali umeendelea kuwasababishia wazazi usumbufu mkubwa katika kumudu gharama za masomo.
Shughuli za kimasomo kama mtihani wa kitaifa wa KCSE, tathmini za KJSEA, KPSEA na KILEA zimekuwa sehemu ya msimu mgumu kwa watoto na wazazi.
Aidha, kashfa nyingine ya kisiasa katika Tume ya Huduma za Walimu (TSC) imetoa taswira mbaya zaidi ya hali ya elimu, ambapo kamishna mmoja anatajwa kutumia mamlaka yake kuingilia uhamisho wa wakuu wa shule kwa lengo la kuwanufaisha wafuasi wake wa kisiasa.
Hali hii imetokea katika Kaunti ya Kisumu, ambapo Mchungaji Charles Ong’injo ametuma barua kwa TSC akitoa onyo kuhusu ushawishi huu wa kisiasa unaoharibu usimamizi wa shule.
Kwa ujumla, hali hii ya ufisadi na ukosefu wa uwajibikaji katika sekta ya elimu ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya elimu nchini Kenya.
Wananchi, hasa wazazi na wadau wa elimu wanahimiza hatua madhubuti zaidi za kuzuia ufisadi, kuboresha uwazi, na kuhakikisha elimu bure na ya lazima inatekelezwa kikamilifu kama ilivyokusudiwa kikatiba