Makala

Gavana wa Tana River Dhadho Godhana agura chama cha ODM

Na STEPHEN ODUOR August 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

GAVANA wa Tana River, Dhadho Godhana, ametangaza mipango ya kuondoka kwenye chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na kuzindua chama chake kipya cha kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027, hatua inayotarajiwa kuchochea kivumbi kikali dhidi ya Seneta Danson Mungatana.

Bw Godhana, ambaye amekuwa mfuasi wa Raila Odinga katika chama cha ODM tangu 2007, alipowania na kushinda kiti cha ubunge wa Galole kwa mara ya kwanza, alisema chama hicho kipya kitawapa wakazi wa Tana River sauti thabiti kitaifa na kukomesha miaka ya kudhulumiwa.

“Kwa miaka mingi serikali imefumba macho kwa matatizo ya Tana River. Viongozi wa kaunti nyingine wanapojadili maendeleo na mgao wa keki ya taifa, sisi hatupati hata makombo,” alisema mjini Hola.

Aliongeza kuwa chama hicho kitaweka wagombea kwa nyadhifa zote mwaka 2027 na akawashutumu maseneta wa sasa na wa zamani kwa kushindwa kuwakilisha masilahi ya wananchi wa kaunti hiyo.

Kulingana na gavana huyo, Kaunti ya Tana River imekuwa ikibaguliwa katika mazungumzo ya maendeleo na kunyimwa hata makombo wenzao wakitoka na minofu.

“Hatuwezi kuwa kila wakati sisi ndio twatumika na kutupiliwa mbali kama tambara bovu, lazima nasi tushike kisu na umma na tukate mnofu kama wengine,” alikiri kwa hisia.

Bw Godhana ametangaza azma ya kuwania useneta kupitia chama hicho kipya, nyadhifa inayomilikiwa na Seneta Danson Mungatana, jambo ambalo limezua cheche za maneno kati yao na kuchemsha siasa katika eneo hilo.

Lakini Bw Mungatana, anayelenga kutetea kiti chake cha useneta, amefutilia mbali mpango huo akisema ni njama ya binafsi ya gavana huyo kukwepa kuwajibika.

“Godhana ndiye janga kubwa zaidi kuwahi kuwapata wakazi wa Tana River katika ngazi ya uongozi. Ni mtu ambaye hakupaswa hata kutokea,” alisema.

Amemshutumu gavana kwa kutofafanua matumizi ya zaidi Sh50 bilioni zilizotolewa kwa kaunti katika hatamu ya uongozi wake.

“Badala ya kuwajibika, anatafuta matawi ya kushikilia. Alete ripoti ya maendeleo yake kwanza, amewafanyia nini Watana katika nyadhifa aliyopewa na pesa alizopewa,” aliongeza.

Hata hivyo, Bw Mungatana amesema yuko tayari kuunga mkono chama cha kanda nzima ya Pwani lakini akashauri kinyume na chama cha kaunti moja, akisema kitaendeleza ukosefu wa mshikamano na kuchochea kubaguliwa zaidi.

“Tusimpe mtu mmoja nafasi ya kusukuma ajenda zake za kibinafsi ambayo itatufanya kutengwa hata hapa Pwani, ni bora kuwa kitu kimoja na wenzetu,” alisema.

Tangazo la Bw Godhana limezua maoni mseto miongoni mwa wakazi.

“Hiki ni chama cha kijiji kisichokuwa na lolote cha maana. Tunahitaji viongozi waunganishe jamii zetu, si kutugawanya zaidi,” alisema Mohammed Komora, mwanafunzi wa udaktari katika Chuo Kikuu cha Makerere.

Katibu Mkuu wa Mtandao wa Asasi za Kiraia Tana River, Rashid James, alimshutumu gavana kwa upendeleo.

“Asilimia themanini ya baraza lake la mawaziri ni jamaa na ndugu zake, kazi zinapewa jamii moja, na watu kutoka nje wanajihisi kama wageni. Hii ni nguo anayoishonea ubabe wake pekee,” alisema.

Mzee Ernest Akumu anaonya hatua hiyo inaweza kuchochea migawanyiko zaidi.

“Kama hii ni kuhusu Tana River pekee, basi si suluhisho. Tunahitaji mshikamo, si ubaguzi,” alisema.

Naye Christine Deye, mtetezi wa haki za wanawake, alisema kaunti haijatatua changamoto za usawa wa kijinsia.

“Viongozi hawajatatua tatizo la upendeleo wa kijinsia. Kuzindua chama sasa hakutafaulu bila mjumuisho. Mpaka pale tutakaposemezana kuhusu kuwa na wabunge wa kike, gavana wa kike, naibu gavana wa kike na seneta wa kike, basi hatuko tayari kwa chama kipya,” alisema.

Hata hivyo, vijana wengine wanaunga mkono wazo hilo wakisema Tana River imesahaulika katika miradi ya kitaifa.

“Miradi ya serikali kuu yote huenda Mombasa, Kwale, Kilifi, lakini Tana husahaulika. Tunahitaji sauti yetu wenyewe,” alisema Stephen Kanumba, kiongozi wa Boda Boda.

Mchambuzi wa siasa Francis Kahindi anasema pambano kati ya Bw Godhana na Bw Mungatana linaweza kubadilisha mwelekeo wa siasa za kaunti hiyo. Hata hivyo, anaonya chama hicho kipya kitakumbwa na changamoto kubwa.

“Siasa za Tana River zinatawaliwa zaidi na misingi ya kikabila, hasa kati ya Wapokomo, Waorma na Wardei. Kwa wapiga kura 164,000 pekee mwaka 2022, chama cha kaunti pekee hakiwezi kustawi kitaifa bila ushirikiano wa kikanda,” alisema.

Bw Kahindi anaongeza kuwa Bw Mungatana anavutia wataalamu na vijana, huku Bw Godhana akitegemea nguvu ya ugavana na uungwaji mkono wa wazee.

Hatua ya gavana Godhana inajiri wakati ODM inapoteza umaarufu Pwani huku baadhi ya viongozi wakihamia vyama vya kikanda au kushirikiana na United Democratic Alliance (UDA) ya Rais William Ruto.

Kujitenga kwa Godhana ni pigo jipya kwa ODM katika ngome yake ya Pwani na kunazua maswali kuhusu nguvu ya chama hicho kufikia uchaguzi wa 2027.

Iwapo chama chake kipya kitakuwa sauti ya waliotengwa au chama cha “kijiji” kwa maslahi yake binafsi, bado ni kusubiri kuona.

Kwa sasa, Tana River inajiandaa kushuhudia mchuano mkali kati ya wana wawili maarufu wa kaunti hiyo katika kinyang’anyiro kitakachokuwa miongoni mwa vitakavyofuatiliwa zaidi Pwani.