Sh58 milioni kutoka kwa CAF si za Harambee Stars
HUENDA kikosi cha Harambee Stars kilichoshiriki soka ya Mataifa Bingwa wa Afrika (CHAN) kikakosa kupata chochote kutokana na zawadi ya Sh58.1 milioni kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kutinga hatua ya robo fainali.
Kulingana na utaratibu wa zawadi, kila timu iliyofuzu kwa robo-fainali ina uhakika wa kupata Sh58 milioni kutoka kwa kiasi cha jumla cha Sh1.3 bilioni kinachogharimia zawadi za mashindano hayo ya wachezaji wanaosakata soka kwenye ligi za nyumbani.
Kulingana na mgawanyo wa tuzo hizo, licha ya kushindwa 4-3 na Madagascar kupitia mikwaju ya penalti baada ya sare ya 1-1 katika muda wa kawaida na ule wa nyongeza, Harambee Stars itapokea mgao wake wa Sh58 milioni, lakini pesa hizo zinatumwa moja kwa moja kwa Shirikisho la Soka la nchini (FKF).
Akiulizwa kuhusu pesa hizo, Rais wa FKF, Hussein Mohammed, alisema watatoa kipaumbele kwa masuala muhimu zaidi, ikiwemo faini ya Sh12.8 milioni waliopigwa kwa ukiukaji kadhaa wa usalama wakati wa mechi za Kundi A jijini Nairobi.
Mohammed alisema wameagizwa kulipa pesa hizo kwa muda usiozidi siku 60, huku akiongeza kwamba baada ya kugharimia mambo muhimu, shirikisho litatoa uamuzi kuhusu kiasi kitakachobakia kutoka kwa mgao huo.
Alipoulizwa kuhusu kiasi kitakachopewa Harambee Stars, Mohammed alisema tayari wametimiza wajibu wao kwa kulipa marupurupu ya wachezaji ambayo yalikuwa Sh21.5 milioni.
“Mafao hayo yote ni juhudi za shirikisho. Tayari tumewalipa Sh21.5 milioni tangu waingie kambini. Kingine chochote kitakachotoka CAF tutajadili na kuamua jinsi kitakavyotumika,” alisema.
Akihojiwa katika kipindi maarufu cha michezo kwenye televisheni, Mohammed alisema kwa jumla Harambee Stars imepokea Sh232 milioni.
Pesa hizo ni pamoja na ahadi ya Rais William Ruto kutokana na matokeo ya kuvutia katika mashindano hayo.
Katika mechi za Kundi A, Harambee Stars ilimaliza bila kushindwa baada ya kuandikisha ushindi wa 1-0 dhidi ya DR Congo, sare ya 1-1 dhidi ya Angola, 1-0 dhidi ya Morocco na 1-0 dhidi ya Zambia, na kufuzu kwa robo-fainali baada ya kuongoza Kundi hilo kwa pointi 10.
Kulingana na utaratibu wa pesa za Rais Ruto, kwa matokeo ya sare, kila mchezaji wa kikosi hicho alipata Sh500,000.
Rais alipandisha kiasi hicho hadi Sh2.5 milioni kwa ushindi wao dhidi ya Zambia ambao uliwawezesha kutinga hatua ya robo-fainali.
Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga pia alimpa kila mchezaji Sh500,000 kwa ushindi huo.
CAF ilitangaza ongezeko la asilimia 75 ya zawadi kwa mshindi ambaye atapata angaa Sh452 milioni, timu itakayomaliza ya pili Sh155 milioni, nafasi ya tatu Sh90.4 milioni na Sh77.5 milioni kwa nafasi ya nne.
Nambari tatu kundi zitapokea Sh38.7 milioni na Sh25.8 milioni kwa kumaliza katika nafasi ya nne kundini.