Makala

KDF wasaka Al-Shabaab waliotoroka wakiwa na majeraha ya risasi

Na KALUME KAZUNGU August 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JESHI la ulinzi (KDF) linaendeleza msako mkali dhidi ya makumi ya magaidi wa Al-Shabaab waliotoroka na majeraha ya risasi, baada ya maficho yao kugunduliwa na kuvamiwa na walinda usalama msituni Boni, Kaunti ya Lamu.

Kwenye uvamizi huo wa Jumanne, KDF wa kitengo maalumu walifaulu kuwaua wanamgambo watano wa Al-Shabaab.

Zana za kivita zinazotumiwa na magaidi, zikiwemo bunduki za aina ya AK-47, mashine za kurushia guruneti kwa mbali (RPGs), taa zinazotumia mianzi ya jua, mahema, risasi na maganda yake pamoja na vifaa vya kuundia vilipuzi vya kutegwa ardhini (IED) pia vilinaswa kutoka kwa wanamgambo hao.

Taarifa kutoka kwa kitengo cha mawasiliano jeshini, ilithibitisha kuuawa kwa Al Shabaab hao watano ilhali wengine wakitokomea msituni wakiwa na majeraha mabaya ya risasi.

“Kikosi maalum cha jeshi letu (KDF) kilikuwa kinatekeleza doria baada ya kupokea taarifa za kijasusi eneo la Lacta Mangai, ndani ya msitu mkuu wa Boni. Kwenye harakati zao walipata kambi ya muda ya Al-Shabaab, ambapo walikabiliana nao na kuwaua watano ilhali wengine wakatoroka na majeraha,” ikasema taarifa hiyo ya jeshi.

Iliongeza kuwa operesheni ya Amani Boni (OAB) iko imara na itaendelea kutia juhudi za kukabiliana na magaidi hadi pale usalama utakaporejelewa na kudhibitiwa vilivyo eneo zima la Boni na viunga vyake.

“Twataka kuhakikisha kila familia ya eneo la Boni inaishi bila hofu. Tunawasihi wananchi kuwa macho na kuripoti shughuli au mtu yeyote mnayemshuku kuwa kero kwa usalama wa kitaifa maeneo yenu ili kufaulisha misheni yetu. Pamoja tutaangamiza ugaidi na kuleta amani ya kudumu eneo la Boni,” ikasema taarifa hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

Mauaji ya magaidi watano wa Al-Shabaab na kujeruhiwa kwa wengine wengi Jumanne yanajiri mwezi mmoja unusu baada ya maafisa watatu wa KDF kuuawa na wengine sita kujeruhiwa kwenye shambulio la kilipuzi cha kutegwa ardhini (IED) eneo la Badaa, karibu na Sankuri msituni Boni.

Shambulio hilo linaloshukiwa kupangwa na Al-Shabaab lilitekelezwa Julai 15, 2025.

Haya yanajiri wakati ambapo serikali kuu imekuwa ikiendeleza operesheni ya kiusalama inayolenga kuwasaka na kuwafurusha au kuwamaliza kabisa magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu mkuu wa Boni.

Operesheni hiyo iliyoanzishwa tangu Septemba 2015 inatekelezwa na KDF kwa ushirikiano na vikosi mbalimbali vya huduma za polisi (NPS) pamoja na utawala (NGAO).

Tangu kuzinduliwa kwake karibu miaka 11 iliyopita, operesheni hiyo imefaulu kushukisha idadi ya visa vya mashambulio, majeruhi na mauaji ya Al-Shabaab ambavyo awali vilikuwa vikirekodiwa Lamu karibu kila siku.