Chungwa la Raila lageuka chungu vigogo wakianza kuondoka
CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM), kinachoongozwa na Raila Odinga, kinaendelea kuyumba huku kikikaribia kuadhimisha miaka 20 tangu kianzishwe, na wakati huo huo kikijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.
Katika matukio ya hivi punde yanayodhihirisha mpasuko unaokikumba chama hicho, viongozi wawili wakuu –Mweka Hazina Timothy Bosire na Gavana Dhadho Godhana wameanzisha harakati za kuunda vyama vipya vya kisiasa, wakilalamikia ukosefu wa usawa na kutengwa katika maamuzi ya chama.
Bosire, ambaye ni mbunge wa zamani wa Kitutu Masaba, amesema analenga kubuni chama kitakachotetea masilahi ya jamii ya Abagusii, akilalamikia ODM kupoteza mwelekeo wa kitaifa.
“ODM sasa imegeuka kuwa chombo cha watu wachache, hakina tena nafasi kwa sauti za mashinani,” alisema Bosire, akithibitisha mipango ya kuanzisha chama kipya.
Kwa upande mwingine, Gavana Godhana wa Tana River ametangaza wazi kuwa atahama ODM na kuanzisha chama kingine kuelekea 2027, akilenga kuwania useneta na kupambana na Seneta wa sasa Danson Mungatana.
“Kwa miaka mingi, Tana River imedhulumiwa. Wakati wenzetu wanagawana minofu ya maendeleo, sisi tunakabidhiwa makombo. Wakati umefika wa sisi pia kushika kisu,” alisema.
Gavana huyo, ambaye aliingia siasa kupitia ODM mnamo 2007, alisema chama chake kitaweka wagombea kwa nyadhifa zote mwaka wa uchaguzi.
Huku hayo yakiendelea, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna ameongoza kundi la wabunge chipukizi kuanzisha vuguvugu jipya la Kenya Moja, wakilenga kupinga ushirikiano kati ya ODM na serikali ya Kenya Kwanza.
Katika ibada ya kanisa la Jesus Teaching Ministry, Nairobi, wabunge kama Antony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini), Babu Owino, Caleb Amisi, na Clive Gisairo, waliapa kushirikiana na viongozi wa upinzani kama Kalonzo Musyoka, Rigathi Gachagua, na Fred Matiang’i kuhakikisha Rais Ruto hatapata muhula wa pili.
“Tunaungana ili kuokoa taifa kutoka kwa utawala dhalimu wa Kenya Kwanza. Tushirikiane na wote wenye maono ya kuikomboa nchi hii,” alisema Kibagendi.
Alidai kuwa zaidi ya wabunge 70 wamejiunga na vuguvugu hilo, ambalo linatarajiwa kusajiliwa rasmi kama muungano wa kisiasa.
Katika ngome ya chama hicho ya Kakamega, uchaguzi wa viongozi wa tawi hilo ulisambaratika wiki jana kutokana na mvutano kati ya kambi za Gavana Ferdinand Barasa na Mbunge Nabii Nabwera (Lugari), waliokosa kuelewana kuhusu mfumo wa uchaguzi.
Mwezi jana, baadhi ya wabunge wa ODM walikosa kuhudhuria mkutano wa wajumbe wa chama ulioitishwa na Raila mjini Kakamega, wakilalamikia “mialiko ya kibaguzi” kutoka kwa Gavana Barasa.
Mchanganuzi wa siasa Martin Andati anasema uasi wa viongozi vijana ndani ya ODM unaonyesha hali ya kutoridhika kutokana na ushirikiano wa chama hicho na serikali.
“Raila alitia saini mkataba na Rais Ruto Machi 7, lakini hakuna kilichotekelezwa. Serikali inaonekana kupuuza makubaliano hayo,” alisema Andati.