Gachagua: Ruto ana faili ya kila anayepatia pesa; wana deni kwake hadi uchaguzi
ALIYEKUWA Naibu Rais, Rigathi Gachagua, amemshambulia vikali Rais William Ruto, akimtuhumu kwa kueneza ufisadi na vitendo vya rushwa ndani ya Bunge.
Akizungumza katika Citizen TV Jumanne, Bw Gachagua alidai kuwa Rais Ruto “hana mamlaka ya kimaadili” kuwalaumu wabunge kwa ufisadi, akisisitiza kuwa yeye ndiye aliyewahonga kwa pesa ili kutekeleza ajenda zake za kisiasa na kisheria.
“Rais hana mamlaka ya kuzungumza kuhusu ufisadi bungeni kwa sababu ndiye aliyefisadi. Ruto hulipa wabunge ili kila anachotaka kifanyike bungeni kipitishwe,” Gachagua alidai.
Alidai kuwa wabunge walilipwa Sh200,000 kila mmoja kuunga mkono Mswada tata wa Fedha wa 2024, huku wale waliopigia kura hoja ya kumwondoa madarakani wakipokea Sh500,000. Aidha, alidai maseneta walihongwa hadi Sh10 milioni kila mmoja.
Zaidi ya hayo, Gachagua alidai kuwa Rais anatumia taarifa za kiusalama kuwabana wanasiasa waliopokea pesa kutoka kwake ili wasimtoroke kisiasa.
“Wale wote waliopokea pesa wakati wa hoja ya kuniondoa mamlakani, wale waliounga mkono Mswada wa Fedha – William Ruto ana faili ya kila mmoja wenu. Kwa pesa mlizochukua, mna deni kwake hadi uchaguzi,” alisema.
Pia alisema kuwa Rais anatumia mashirika ya serikali kama Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA) na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuwatisha wabunge wanaokataa kuhongwa.
“Ikulu ni uwanja wa uhalifu. Naibu Rais anatembea na magunia ya pesa, akihonga wanawake na vijana ili wapige kelele za ‘mihula miwili’. Kisha Rais anajifanya kupigana na ufisadi. Ataanzia wapi?” aliuliza Gachagua.
Kiongozi huyo wa chama cha DCP pia alifichua kuwa aliwahi kusaidia kupanga Rais Ruto kukutana na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo almaarufu Hemedti, kiongozi wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) cha Sudan, wakati alipokuwa Naibu Rais.
Alidai kuwa mkutano huo ulitokea kwa ombi la Ruto, kwa kuwa rais aliye madarakani hawezi kwa kawaida kumualika naibu wa nchi nyingine.
“Ruto ana uhusiano wa karibu na Hemedti. Mimi ndiye niliyemwalika Hemedti kwa ombi la Ruto, kwa sababu kidiplomasia, rais hawezi kumwalika naibu wa nchi nyingine. Wakati huo Hemedti alikuwa Naibu Rais wa Sudan,” alieleza.
Gachagua alisema kuwa alipewa barua rasmi ya kumwalika Hemedti, akamchukua uwanjani, akamfikisha kwa Ruto na wakashiriki mazungumzo yao.
“Mazungumzo yao yalihusu biashara, dhahabu na uhusiano wa kiuchumi,” alifichua.
Gachagua pia alitaka Rais ajibu tuhuma kuhusu uhusiano wake na kundi la kigaidi la Al-Shabaab, akipuuza madai ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, kwamba anachafua jina la nchi na huduma ya polisi.
“Murkomen si msemaji wa Ruto. Rais anaweza kueleza kama alikutana au hakukutana na Al-Shabaab,” alisema.
Aliweka wazi kuwa hakuwahi kuwaita wakazi wa Mandera magaidi, bali alikuwa akimtaka Rais kufafanua tuhuma hizo.
“Wakazi wa Mandera hawahusiki na tuhuma hizi. Nilimtaka Ruto ajibu madai ya kukutana na Al-Shabaab, si watu wa Mandera,” alieleza.
Gachagua pia alikana kuwa yeye ni kiongozi wa kikabila, akisema Rais Ruto ndiye anayesuka propaganda dhidi yake baada ya kutofautiana kisiasa.
“William Ruto ni mtaalamu wa kusuka propaganda. Tulipokuwa marafiki, alinisifu kama mtu mzuri, mwanamikakati wa kisiasa na mpenda watu. Lakini tulipotofautiana, akanigeuza kuwa mkabila,” alisema.
Akitoa mfano wa Uchaguzi Mkuu wa 2022, Gachagua alisema yeye na jamii yake walimpigia Ruto kura kwa asilimia 87.
“Kama ningekuwa mkabila, ningemsikiliza Uhuru Kenyatta aliponiambia nimuunge mkono Raila. Lakini niliamua kumuunga mkono Ruto, hata kama hakuwa Mkikuyu,” alisema.
Alishangaa kwa nini jamii ya Ruto haikumpa Raila kura hata moja, akisema hilo linaonyesha ukabila ulikuwa upande wa Rais.
Gachagua alitoa changamoto kwa Rais na wandani wake watoe ushahidi wa video au sauti inayomuonyesha akitoa matamshi ya chuki dhidi ya jamii nyingine.
“Naitaka serikali ya Ruto iwakilishe ushahidi wowote unaoonyesha nimetukana au kudhalilisha kabila lolote. Mimi ni mzalendo halisi,” alisisitiza