Uporaji wa SHA: Wabunge waambia Duale ‘aache kizungu mingi’ ajiuzulu
BAADHI ya wabunge wamempa Waziri wa Afya Aden Duale makataa ya saa 48 kujiuzulu, wakdai ni mmoja wa wahusika wakuu katika kashfa ya ufisadi ya mabilioni ya pesa ndani ya Mamlaka ya Bima ya Afya ya Jamii (SHA).
Iwapo Duale hatajiuzulu kufikia mwisho wa muda huo, wabunge hao wametishia kuanzisha hoja ya kumtimua.
“Iwapo ndani ya saa 48 hadi 72 Duale hatajiuzulu, tutawasilisha hoja ya kumtimua kuhakikisha anaondolewa kazini,” alisema Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini).
Wakizungumza kwa hasira, wabunge hao wanachama wa vuguvugu la Kenya Moja Alliance walidai kuna ufisadi katika SHA na kama waziri anayesimamia Wizara ya Afya, Bw Duale anafaa kujiuzulu.
Bw Kibagendi aliandamana na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Clive Gisairo (Kitutu Masaba) na Wilber Oundo (Funyula).
Hata hivyo, Duale Jumatatu, Agosti 26, alifichua kuwa SHA imekuwa ikipoteza pesa kupitia mbinu ghushi kama vile, wagonjwa hewa.