NMG yakubaliwa kumpima akili mwanamume aliyeiba magazeti yake mitandaoni
MAHAKAMA moja ya Nairobi Alhamisi, Oktoba 28, 2025 ilikubalia kampuni ya Nation Media Group Plc (NMG) kumteua daktari kushiriki katika zoezi la kupimwa kwa akili mwanamume anayeshtakiwa kughushi mtandao wa e-paper bila idhini.
Hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Geoffrey Onsarigo aliruhusu NMG kumteua daktari kushiriki na kushuhudia zoezi la kupimwa akili kwa Calvin Kinyanjui Kung’u katika hospitali ya Mbagathi.
Bw Onsarigo aliamuru Kung’u arudishwe hospitali ya Mbagathi akafanyiwe ukaguzi kamili.
Agizo hilo lilitolewa kufuatia ufichuzi wa kiongozi wa mashtaka Bi Wanjiru Waweru kwamba “ripoti aliyokabidhiwa kutoka Mbagathi sio kamilifu.”
Bi Waweru alisema hospitali hiyo iliomba muda zaidi hadi Septemba 4, 2025 kukamilisha zoezi hilo.
Wakili wa NMG Kelvin Onyango aliomba mahakama iamuru kampuni hiyo kubwa zaidi Afrika ya Kati na Mashariki ikubaliwe kumteua daktari kushiriki katika upimwaji wa Kung’u.
Naye wakili wa mshtakiwa aliomba mahakama iruhusu mama yake mshtakiwa afike hospitalini humo kutoa taarifa muhimu kuhusu mshtakiwa.
Na wakati huo huo, mshtakiwa aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana ikitiliwa maanani adhabu ya kosa analoshtakiwa kufanya ni Sh10,000.
Akitoa uamuzi, Onsarigo alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh100,000 na kuamuru kesi inayomkabili itajwe Septemba 8, 2025.
Kung’u alikataa kujibu mashtaka mawili dhidi yake aliposhtakiwa Agosti 25, 2025 akidai anaugua maradhi ya akili.
Bi Waweru aliomba mshtakiwa apelekwe Mbagathi kupimwa iwapo yuko na matatizo ya akili kabla ya kusomewa mashtaka.
Kung’u alishtakiwa pamoja na Jackson Wangigi Kariuki kwa kuiba kutoka mtandao wa e-Paper wa NMG magazeti ya Taifa Leo, Daily Nation, Business Daily na The East African kinyume cha sheria za umiliki wa haki.
Jackson alikabiliwa na mashtaka mawili kwamba kati ya Juni 23 na Julai 10, 2025 aliuza kidijitali magazeti ya Taifa Leo, Daily Nation, Business Daily na The East African.
Alikana kutumia mtandao wake wa WhatsApp uliosajliwa na kampuni ya Safaricom kupitia nambari yake ya simu 0702976857.
Hakimu alielezwa na kiongozi wa mashtaka kwamba Calvin alikaidi haki za uuzaji wa kampuni ya Nation Media Group PLC na kuiba kwa kuuza magazeti yake mitandaoni bila idhini.
Kesi itatajwa Septemba 8, 2025 mahakama ielezwe ikiwa Calvin atajibu mashtaka au la.