Habari

Korti yazima ujenzi wa ‘kanisa la Ruto’ katika ikulu zote

Na JOSEPH WANGUI August 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu imeamuru kusitishwa kwa muda ujenzi wa kanisa la kudumu au jengo lolote la kidini katika majengo ya Ikulu, Nairobi.

Agizo hilo la muda pia linazuia ujenzi kama huo katika Ikulu za Rais zilizoko maeneo mbalimbali nchini.

“Agizo la muda linatolewa kuizuia Serikali ya Kenya, maafisa wake, au yeyote kwa niaba yao, kujenga kanisa la kudumu au jengo lolote la kidini katika Ikulu ya Nairobi au katika Ikulu nyingine yoyote hadi Novemba 18, 2025,” alisema Jaji Chacha Mwita.

Agizo hilo lilitolewa kufuatia kesi iliyowasilishwa na mashirika manne ya kijamii – Transparency International Kenya, Kenya Human Rights Commission, Inuka Kenya ni Sisi, na The Institute of Social Accountability – yaliyopinga hatua ya Rais William Ruto kuanzisha ujenzi wa kanisa ndani ya Ikulu ya Nairobi.

“Baada ya kuzingatia hoja za kesi na dharura ya jambo hili, ninaona kuwa ombi na kesi kuu zimeibua masuala muhimu ya kikatiba na kisheria yanayohusu uhusiano wa dini na serikali,” alisema.