Engonga, aliyepata umaarufu sababu ya filamu za ngono, agongwa miaka 8 jela
MPWA wa Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Obiang Nguema, ambaye mwaka jana alihusishwa na kashfa ya video za ngono, amehukumiwa kifungo cha miaka minane gerezani kwa kosa la ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.
Baltasar Ebang Engonga, aliyekuwa mkuu wa Shirika la Kitaifa la Uchunguzi wa Kifedha, alipatikana na hatia ya kutumia fedha za serikali kwa matumizi binafsi, kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama.
Engonga, anayejulikana kwa jina la utani la “Bello” kutokana na sura yake ya kuvutia, alipata umaarufu hasi mwaka jana baada ya video kadhaa kusambaa mtandaoni zikimuonyesha akifanya mapenzi na wanawake tofauti — wakiwemo wake wa watu na jamaa wa watu waliokaribu na uongozi wa taifa hilo.
Video hizo zilisambazwa wakati Engonga alikuwa kizuizini, akikabiliwa na tuhuma za kuhamisha kiasi kikubwa cha pesa alizoiba hadi kwenye akaunti za siri katika visiwa vya Cayman.
Engonga alipatikana na hatia pamoja na maafisa wengine watano wa serikali waliodai malipo ya safari kwa njia ya udanganyifu, ambapo kiwango cha fedha walichojipatia kilikuwa kati ya dola 9,000 (Sh1.3 milioni) hadi dola 220,000 (Sh32 milioni).
Kukamatwa kwa Engonga mwezi Oktoba mwaka jana na kufedheheshwa hadharani kulitafsiriwa na wachambuzi kama njama ya kumuangamiza kisiasa, kwani alitajwa kuwa mmoja wa watu waliokuwa na matumaini ya kumrithi mjomba wake kama rais wa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.
Rais Obiang, ambaye ni kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi duniani tangu mwaka wa 1979, tayari amemteua mwanawe, Teodoro Obiang Mangue, kuwa makamu wa rais — hatua iliyozua maswali kuhusu urithi wa uongozi wa taifa hilo.
Ingawa hapo awali Engonga alikuwa miongoni mwa waliokuwa wakichunguza uhalifu wa kifedha kama vile ulanguzi wa fedha alijikuta katika gereza hatari la Black Beach jijini Malabo baada ya kushtakiwa kwa ufisadi.
Simu zake na kompyuta zilichukuliwa na maafisa wa usalama, na siku chache baadaye video za faragha zilianza kusambazwa mtandaoni kwa wingi.
Uhalisia wa video hizo haujathibitishwa rasmi, lakini kwa kuwa vifaa hivyo vilikuwa mikononi mwa maafisa wa usalama, kuna mashaka kuwa ni mtu kutoka ndani ya mfumo wa usalama aliyezisambaza — huenda kwa lengo la kuharibu jina na sifa ya Engonga.
Mbali na kifungo, mahakama pia ilimhukumu Engonga kulipa faini ya dola 220,000 (takribani Sh32 milioni), kwa mujibu wa msemaji wa Mahakama Kuu, Hilario Mitogo, aliyenukuliwa na shirika la habari la AFP kupitia ujumbe wa WhatsApp kwa wanahabari.