Hofu ya Gachagua kuongea bila breki; viongozi wa upinzani watahadharishwa, ‘hana siri!’
ALIYEKUWA Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua, ameibua mjadala tata kisiasa kwa tabia ya kutoa madai ambayo anasema ni ufichuzi wa shughuli za ndani za serikali aliyohudumia.
Hii ni hatua inayokiuka kiapo cha kutunza siri za utumishi wa umma.
Katika kauli yake ya hivi majuzi, alidai kuwa Rais anatumia mashirika ya serikali kama Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA) na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuwatisha wabunge wanaokataa kuhongwa na kwamba, alitumwa na rais kumwalika kiongozi wa kundi la waasi nchini Sudan.
Kiongozi huyo wa chama cha DCP alidai kuwa aliwahi kusaidia kupanga Rais Ruto kukutana na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo almaarufu Hemedti, kiongozi wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) cha Sudan, wakati alikuwa Naibu Rais.
Alidai kuwa mkutano huo ulitokea kwa ombi la Ruto, kwa kuwa rais aliye madarakani hawezi kwa kawaida kumualika naibu wa nchi nyingine.
“Ruto ana uhusiano wa karibu na Hemedti. Mimi ndiye niliyemwalika Hemedti kwa ombi la Ruto, kwa sababu kidiplomasia, rais hawezi kumwalika naibu wa nchi nyingine. Wakati huo, Hemedti alikuwa Naibu Rais wa Sudan,” alieleza.
Gachagua alisema kuwa alipewa barua rasmi ya kumwalika Hemedti, akamchukua JKIA, akamfikisha kwa Ruto na wakashiriki mazungumzo yao.
Ingawa haikuweza kuthibitishwa, kauli hiyo, sawa na nyingine ambazo amekuwa akitoa, imezua mjadala mkali, huku wachambuzi wa siasa na usalama wakihusisha kitendo hicho na ukiukaji wa kiapo cha kutunza siri za utumishi wa umma, kama inavyosema Katiba ya Kenya na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Kwa mujibu wa sheria, maafisa wa umma wana wajibu wa kudumisha siri za serikali, hasa zile zinazohusu diplomasia, usalama wa taifa na masuala nyeti ya kitaifa. Anayeikiuka yumo hatarini kusukumwa jela hadi miaka 14.
Aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu, ametoa onyo kwa viongozi wa upinzani wanaoshirikiana na Gachagua, kwamba hawezi kutunza siri zao.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook mnamo Jumatano, Agosti 27, 2025, Wambugu – ambaye awali alikuwa mshirika wa karibu wa Gachagua – alisema ingawa ni jambo la kutia moyo kuona upinzani ukikutana, ni lazima wawe waangalifu wanaposhirikiana na Gachagua.
“Naona viongozi wa upinzani walikutana leo. Ni vyema. Tunawakumbusha kuwa waangalifu na mazungumzo yoyote wanayofanya wakiwa na Gachagua. Ndani ya miaka miwili ijayo, tutapewa taarifa zote kuhusu walichojadili kwa undani,” aliandika Wambugu.
Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, alithibitisha kupitia ukurasa wake rasmi kuwa, alikutana na Gachagua, pamoja na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi.
Kulingana na Kalonzo, viongozi hao walitumia muda huo kushirikiana na kubadilishana mawazo.
Kalonzo pia alifichua kuwa mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi mashuhuri wa upinzani walioungana, wakiwemo kiongozi wa DAP-K, Eugene Wamalwa, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, na Saitoti Torome.
Lengo kuu la mkutano huo, Kalonzo alisema, ni kuimarisha kampeni ya Wantam, inayolenga kumwondoa Rais William Ruto mamlakani ifikapo mwaka wa 2027.
Ingawa baadhi wanaona hatua ya Gachagua kuungana na viongozi wa upinzani kama ishara ya kushirikiana kwa dhati, onyo la Wambugu linaonyesha tahadhari kuhusu uaminifu wa kisiasa na siri tza mikutano hiyo kuvuja baadaye.
Kulingana na mchanganuzi wa siasa na masuala ya utawala Dkt Francis Limo, Bw Gachagua amekuwa akivuka mipaka katika kushambulia serikali.
“Kumbuka, alipokuwa serikalini alilaumu maafisa wa Huduma ya Taifa ya Ujasusi (NIS) akidai hawakumshauri rais ipasavyo na juzi akiwa Amerika, alitoa kauli ambazo, afisa wa umma hafai kuonekana hata kuwazia kutoa si tu ugenini bali hata nyumbani,” alisema Dkt Limo.
Bw Gachagua amekuwa akijitetea akisema, anachofichua ni ukweli na ni ukweli wake uliofanya atimuliwe serikalini.
Kulingana na Bw Wambugu, Gachagua hazuii ulimi wake.
“Kuna tofauti kubwa kati ya kusema ukweli na kutozuia ulimi. Gachagua ameonyesha hana breki za ulimi kabisa,” aliandika Wambugu.