Kura: Ruto, Uhuru, Gachagua na Muturi kupimana nguvu Mbeere Kaskazini
KAMPENI za kumrithi aliyekuwa Mbunge wa Mbeere Kaskazini, Geoffrey Ruku, zimeingia hatua muhimu huku wagombea wanne wakitangazwa rasmi na kuashiria mapambano makali kati ya serikali na upinzani.
Kiti hicho kilibaki wazi baada ya Bw Ruku kuteuliwa Waziri wa Huduma za Umma na Rais William Ruto.Wagombeaji ni Leonard Muthende, mgombea wa chama tawala cha UDA; Duncan Mbui anayepeperusha bendera ya chama kipya cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua; Newton Kariuki almaarufu Karis anayeungwa mkono na Democratic Party (DP) inayoongozwa na aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa na waziri Justin Muturi; na mfadhili maarufu Jacob Ireri Mbao wa tikiti ya Jubilee inayoongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Ingawa kuna majina manne kwenye orodha, wachanganuzi wa siasa wanaamini kuwa ushindani wa kweli utakuwa kati ya muungano wa upinzani na serikali kupitia UDA.
Tayari tetesi zimeanza kuibuka kuwa upinzani unaweza kwa makusudi kuwasilisha wagombea zaidi ili kugawanya kura za UDA. Lakini kwa sasa macho yote yameelekezwa kwa Bw Mbui na Bw Kariuki kama wanasiasa wa upinzani wenye kupigiwa upatu zaidi.
Bw Mbui ni MCA wa sasa wa wadi ya Evurori yenye wapiga kura wengi zaidi katika eneobunge hilo.Anahudumu muhula wake wa pili, na ana ushawishi mkubwa wa kisiasa kule mashinani.
Kwa upande mwingine, Bw Kariuki – ambaye pia ni mwanamuziki – ni MCA wa muhula wa tatu wa wadi ya Muminji, na anafahamika kwa uzoefu wake na uwezo mufti wa kusoma mawimbi ya siasa yanavyopiga katika wadi na eneobunge kwa jumla.Lakini mgombea wa UDA, Bw Muthende anayefahamika kwa jina maarufu Leo, si mtu wa kubezwa.
Anatokea wadi ya Nthawa na ana mitandao mizito katika eneo zima, shususan kutokana na kampeni yake ya ugavana wa Embu mwaka 2017 kupitia chama cha Narc Kenya ingawa hakufanikiwa.Bw Muthende anaungwa mkono na serikali ya kitaifa pamoja na mtandao wa kisiasa wa Waziri Ruku, na inadaiwa anajizatiti kuhakikisha kiti kinabakia mrengo wa serikali.
Wanaomfahamu bw Leo wanamtaja kama “mpanga mikakati kimyakimya” ambaye alihusika kwa karibu katika ushindi wa Bw Ruku katika uchaguzi mkuu wa 2022.Wachanganuzi wanasema kuwa kama MaBw Mbui na Kariuki watakataa kuachia mmoja wao, basi UDA itaibuka mshindi kwa urahisi.
‘Hesabu ni rahisi: wagombea wawili wa upinzani kwenye debe humaanisha UDA itashinda kwa urahisi. Lakini kama upinzani utaungana, basi hapo kuna pambano la kweli,’ alisema mchanganuzi mmoja wa siasa.
Matarajio sasa yako kwa viongozi wa vyama husika – Justin Muturi (DP), Rigathi Gachagua (DCP), na Lenny Kivuti wa Devolution Empowerment Party (DEP) – ambao wana nafasi ya kuwalazimisha wagombea wa upinzani kuafikiana.
Wakati huohuo, Jacob Mbao, ambaye anaheshimika kutokana na kazi zake za hisani na uthabiti wake licha ya ulemavu wa kusikia, anaweza kushawishiwa kuachia mgombea wa pamoja wa upinzani. Hata hivyo, ameonekana akiendelea na kampeni zake kote eneo bunge hilo akisema kuwa
“Mbeere Kaskazini inahitaji sura mpya ya uongozi na yeye ndiye suluhisho.”Joto la kisiasa katika Mbeere Kaskazini tayari imeanza kupanda huku kila kambi ikiimarisha mikakati kushindana kwenye debe.Hivi majuzi, Naibu Rais Kithure Kindiki aliahidi kukita kambi Mbeere Kaskazini kuhakikisha UDA inatwaa kiti hicho.