Habari za Kitaifa

Walia kwa majuto baada ya kuuza figo zao

Na TITUS OMINDE, BARNABAS BII August 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Waathiriwa wa madai ya biashara haramu ya figo inayohusishwa na Hospitali ya Mediheal wamejitokeza hadharani na kutoa simulizi za kusikitisha kuhusu walivyodhulumiwa, huku Kamati ya Afya ya Bunge ikifanya uchunguzi jijini Eldoret.

Amon Kipruto, mwenye umri wa miaka 23 kutoka mtaa wa Kipkenyo, Kaunti ya Uasin Gishu, aliiambia kamati hiyo kwamba, alidanganywa mnamo Mei 2024 kuwa kuna nafasi ya kupata pesa nyingi kwa kutoa figo.

“Nilikutanishwa na mtu wa asili ya Kihindi aliyesema kuwa ni salama kutoa figo. Siku ya kwanza alinipa Sh50,000,” alisema Kipruto, ambaye ni mwanafunzi aliyeacha shule kutokana na hali ngumu ya kifamilia.

Alisema alipelekwa Hospitali ya Mediheal kufanyiwa uchunguzi wa kiafya, na baadaye kuthibitishwa kuwa anafaa kutoa figo. Hata hivyo, kabla ya upasuaji, alipewa kitambulisho bandia kikionyesha kuwa yeye ni raia wa Somalia aitwaye Mohammed Kipruto.

“Walichukua kitambulisho changu halisi na kunipa bandia wakisema niseme kuwa natoka Mogadishu, ili kuepuka unyanyapaa,” alieleza. Baada ya upasuaji, alipokea Sh400,000 zaidi na kisha akatoroka.

Familia yake iliporipoti kwamba alikuwa ametoweka, alijitokeza siku chache baadaye akiwa mgonjwa na mwenye huzuni.Mama yake, Sarah Jeruto, mwenye umri wa miaka 46, alisema walipompeleka katika Hospitali ya Moi (MTRH), madaktari walithibitisha figo moja ilikuwa imeondolewa.

“Mwanangu hakuwa hivi. Sasa huwa mgonjwa kila wakati. Tunahitaji haki,” alisema Bi Jeruto kwa huzuni baada ya kuhojiwa na wanahabari katika hoteli ya Boma Inn mjini Eldoret.

Emmanuel Kipkosgei, mwathiriwa mwingine aliyedai kudhulumiwa, alisema aliahidiwa Sh1.2 milioni kwa kutoa figo lakini alipewa nusu ya fedha hizo pekee.“Baada ya upasuaji, nilipewa Sh600,000. Wakasema salio ningepewa baadaye. Hadi leo sijaona pesa hizo. Badala ya kuwa tajiri, maisha yangu yamezidi kuwa magumu,” alisema Kipkosgei.

Mama yake, Leah Jepkorir, alithibitisha kuwa matokeo ya hospitali pia yanaonyesha figo ya mwanawe ilitolewa.“Tunaiomba serikali iingilie kati. Mwanangu sasa ni mgonjwa milele,” alilalama.Kamati ya Bunge kuhusu Afya, ikiongozwa na Mbunge wa Seme Dkt James Nyikal, ilizuru Eldoret kusikiliza ushahidi kutoka kwa waathiriwa, polisi, na wahudumu wa afya.

“Tunasikiliza ushahidi na tutatoa mapendekezo kuhusu hatua ya kuchukuliwa,” alisema Dkt Nyikal.Mbunge wa Nandi Hills, Benard Kitur, alidai maisha yake yako hatarini baada ya kufichua kashfa hiyo, akisema baadhi ya maafisa wakuu wa polisi wanawalinda wahusika.

Biashara ya viungo vya binadamu ni haramu nchini Kenya, na mtu anaruhusiwa tu kutoa figo kwa hiari kwa ndugu yake wa damu. Licha ya hayo, kuna ripoti kuwa watu maskini wamekuwa wakilengwa na mitandao ya wahalifu inayofanikisha biashara hiyo.

Mwanzilishi wa Hospitali ya Mediheal, Dkt Swarup Mishra, ambaye pia alikuwa Mbunge wa Kesses, amekanusha kuhusika na biashara hiyo haramu.

“Naunga mkono uchunguzi wa kina. Kama nitapatikana na hatia, niko tayari kubeba lawama,” alisema awali.Wakili wa hospitali hiyo, Bw Katwa Kigen, aliambia kamati kuwa Mediheal imefanya upasuaji wa figo 476 tangu 2018 – 371 kwa Wakenya na kwa wageni 105 na iko tayari kutoa rekodi zote.

“Tumekuwa tukifuata taratibu zote za kisheria. Ada yetu ni Sh3.2 milioni kwa Waafrika na Sh4.5 milioni kwa wageni. Gharama hii ni ndogo ikilinganishwa na nchi za nje,” alisema Dkt Mishra.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Afya Duniani (WHO) tayari yameelezea wasiwasi kuhusu biashara haramu ya viungo vya binadamu, yakisema huathiri zaidi watu maskini katika nchi zinazoendelea.

Mnamo 2019, Wizara ya Afya ya Kenya ilizindua kitengo cha kusimamia uchangiaji damu na upandikizaji wa viungo. Hata hivyo, utekelezaji wa sheria hiyo bado unasuasua.

Dkt Nduku Kilonzo wa Huduma za Kitaifa za Damu alisema wanaendelea kuandaa mfumo wa kusaidia uchangiaji wa viungo kwa usalama na kwa mujibu wa sheria