Ruto, Raila waachiana viti chaguzi ndogo na kuacha Upinzani umeduwaa
RAIS William Ruto wa UDA na Kinara wa ODM Raila Odinga, wamekubali kuwa vyama hivyo viwili vitakuwa na mwaniaji moja katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ugunja Kaunti ya Siaya.
Jumapili, Rais Ruto alisema UDA imekubali kuwa itamuunga mkono mwaniaji wa ODM ili kuzuia mikwaruzano kati ya vyama hivyo viwili ambavyo vipo ndani ya Serikali Jumuishi.
Kiti cha eneobunge la Ugunja kilisalia wazi baada ya Opiyo Wandayi kuteuliwa kama waziri wa Kawi.
Taifa Leo imebaini kuwa UDA huenda pia ikakubali kuondoa mwaniaji wake Kasipul na Magarini ambapo washikilizi wake walikuwa wa ODM.
Eneobunge la Kasipul lilisalia wazi baada ya Ong’ondo Were kupigwa risasi na kuuawa kinyama mnamo Apili mwaka huu jijini Nairobi.
Magarini nayo haijakuwa na mbunge baada ya ushindi wa Harrison Kombe kufutwa na Mahakama ya Juu.
“Nyinyi watu mnafahamu kuwa kutakuwa na uchaguzi mdogo eneobunge hili kwa sababu nilimteua mwakilishi wenu kuwa waziri wa kawi,
“Tumekubaliana kuwa UDA haitakuwa na mwaniaji na sote tutakuwa na mgombeaji ambaye anaungwa mkono na UDA na ODM,” akasema Rais William Ruto katika eneobunge la Ugunja Jumapili.
Kauli ya Rais ilikuja wakati ambapo UDA ilikuwa imetangaza kuwa ingekuwa na mgombeaji kwenye chaguzi ndogo hata maeneo ambayo ODM ilikuwa ikishikilia viti.
Bodi ya Uchaguzi ya UDA ilikuwa imetangaza kuwa ingewasilisha wawaniaji kwenye chaguzi ndogo sita za ubunge, moja ya useneta pamoja na maeneo 16 ya uwakilishi wadi.
Chaguzi nyingine ndogo zitaandaliwa Mbeere Kaskazini, Malava na Banisa pamoja na uchaguzi wa useneta wa Baringo.
Imebainika kuwa kama njia ya kurudisha mkono, ODM nayo haitakuwa na wawaniaji Banisa, Malava na Mbeere Kaskazini pamoja na Kaunti ya Baringo pamoja na wadi nyingine 13.
Banisa ilibakia wazi baada ya mauti ya Hassan Kullo nayo Malava ikabakia bila mbunge baada ya Malulu Injendi pia kufariki dunia.
Kule Mbeere Kaskazini, kiti kilisalia wazi baada ya Geoffrey Ruku kuteuliwa kama waziri wa utumishi wa umma.
“Kamati ya ODM imeafikiana kuwa itawasilisha wawaniaji kwenye chaguzi zote ndogo isipokuwa saba kati ya 23,” ikasema ODM.
Vivyo hivyo, Bodi ya UDA ilikuwa imewaalika wawaniaji wachukue fomu ya kuwania uchaguzi huo mdogo na walikuwa wameweka Septemba 20 kama siku ya kuandaliwa kwa mchujo.
“Wanaotaka kusimama wajisajili kupitia mtandao wa UDA,” akasema Mwenyekiti wa UDA Anthony Mwaura.
Rais Ruto atakuwa akilenga kuonyesha kuwa bado umaarufu wake uko juu hasa Mbeere Kaskazini, Malava na Baringo.
Kwa upande mwingine ODM itakuwa ikilenga kuonyesha Raila bado anadhibiti ngome zake za kisiasa.